HADITHI
ZA KINDIJA
Kitabu
hiki ni kitabu cha kwanza katika mfululizo wa hadhithi za Fasihi simulizi zenye
utamu na mtiririko wa kuvutia toka kwa Ndugu James Kalimanzila. Kutokana na
vijana wengi leo kutokuwa na utambuzi wa mila na tamaduni zetu za kitanzania
wamejikuta wakiuvaa usasa na kutembea chini ya mwamvuli wa utandawazi na kuhisi
hapo ndio mwisho wa maisha.
Maisha
huwa hayawezi kwenda mbele bila ya kukumbuka yalikotoka. Ndio maana vijana
wengi hata waliosoma hawasikii furaha ya moyoni kwa sababu mila na desturi zao
ndizo zilikusudiwa kuwapa furaha mioyoni mwao. Hapa mwandishi amekusudia
kuwakumbusha japo kwa uchache baadhi ya mila na desturi za kisukuma kwa wale
walioanza kusahau au kwa wasio na utambuzi kabisa na mila na desturi hizo.
Aidha mwandishi wa kitabu hiki ameamua pia
kutia kalamu yake katika uandishi wa kazi za Fasihi kutokana na mahitaji
makubwa yaliyopo kwenye kazi za Fasihi. Mahitaji haya ni pamoja na kuinua
kiwango cha ujuzi wa lugha na uwezo wa kusoma na kufahamu. Ni dhumuni mahususi
la mfululizo wa vitabu hivi kuimarisha maadili ya wasomaji wake kwa kuinua ubunifu,
udadidisi, bidii, uaminifu, utiifu na kuhuisha mapenzi ya dhati.
Hadithi
zote zimeandikwa kwa njia ya kuwavutia na kuwapendeza wasomaji pamoja na kuwapa
mafunzo yafaayo. James Kalimanzila ambaye ni mwandishi na mtunzi wa
kitabu hiki amewahi kutunga na kuandika kazi nyingi kama: Flip-flop of
labour shortage pamoja na Palaysed digital economy. Aidha katika
kuandaa kazi hii ameshirikiana na ndugu Godlove Dismas Ngowella, Mwalimu
na mtaalam wa fasihi ya Kingereza.
HADITHI
1. MZIMU WANGU.
Kulikuwa
na kijana aliyejulikana kwa jina la Dongwe, kijana huyu alizaliwa katika kijiji
cha Kanyaga kilichopo mashariki mwa Wilaya ya Kahama. Kijiji cha Kanyaga kina
madhari ya milima ya mawe makubwa, mapango, misitu minene, mito yenye kina
kirefu na mabwawa ya maji. Wanakijiji wa Kanyaga walikuwa wafugaji wa mifugo
kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda. Walikuwa wakijishughulisha pia na
shughuli za kilimo cha mazao kama vile mahindi, maharagwe, njugu mawe, karanga,
mihogo, miwa na mpunga.
Wanakijiji
wa Kanyaga walikuwa wakiamini katika mila na desturi za Uswega ambazo walizirithi kutoka kwa mizimu ya babu zao. Katika
kuhakikisha kuwa mila na desturi za kijiji hiki zinatunzwa na kurithishwa kwa
vizazi vijavyo kulikuwa na desturi ya kumrithi uongozi kiongozi aliyefariki.
Vigezo vya urithi vilitaka kijana wa kiume, kipenzi cha marehemu baba yake na
kipenzi mizimu pia.
Nchemu,
baba yake na Dongwe ndiye aliyekuwa kiongozi kwa miaka Zaidi ya 100. Nchemu
alirithi uongozi huu kutoka kwa baba yake aliyeitwa Doi aliyefariki akiwa na
umri wa miaka 115. Kwa ufupi familia ya Dongwe ndio ilikuwa familia ya kitemi
pale kijijini. Familia ya kitemi ndiyo ilikuwa ikihusika na kwenda kuongoza
ibada za matambiko ya kimila kwa ajili ya kuomba Amani, mvua, kutoa mikosi kama
ya kuvamiwa na wadudu waharibifu wa mazao aina ya nzige na mabuu.
Kijana
Dongwe alipendwa sana na wazazi wake hasa baba yake huku akiwa ni kijana pekee
wa kiume aliyebakia baada ya kaka yake kufariki kwa kula uyoga wa sumu. Wabeba
mikoba, waliokuwa wakimsaidia Ntemi, walihakiki kuwa Dongwe ndilo chaguo la
mizimu kwa sababu licha ya kula uyoga wenye sumu wakiwa pamoja na kaka yake,
kijana huyu hakudhurika hata kidogo. Hii ilisemwa kuwa ni ulinzi madhubuti wa
mizimu juu yake kwa sababu ndiye aliyepaswa rithi mikoba ya baba yake.
Dongwe
alipotimiza umri wa miaka 10 Baba yake alifariki dunia kutokana na magonjwa ya
uzee yaliokuwa yakimkabili, kwani alikuwa amefikisha umri ya miaka 130. Msiba
huu ulikuwa pigo kubwa kwa kijana Dongwe, alilia usiku na mchana akifirikiri
labda machozi mengi yangeweza kuwa tiba ya baba yake kuamka. Haikuwa vile
alivotaka yeye maana siku ya tatu baba yake alifukiwa na kifusi cha udongo na
kuwekewa maua juu ya kaburi na baadaye kumwangwa damu ya kondoo juu ya kaburi
lake. Alikumbuka namna baba yake
alipotuma walinzi wake waende kumchagulia vazi zuri na viatu vya makata mbuga, magurudumu ya gari, siku
ya gurio. Vazi na makata mbuga
vilikuwa zawadi ya mwisho ya baba yake na ndivyo alivyokuwa amevaa wakati wote
wa msiba wa baba yake.
Kijana Dongwe alisikitika sana hasa
alipokumbuka namna alivyopendwa na Baba yake na namna yeye mwenyewe
alivyompenda baba yake. Lakini pia alibaki kuwa na huzuni Zaidi kiasi cha
kukosa hamu ya kula na usingizi kumpaa mara baada ya kugundua kuwa yeye ndie
aliyetakiwa kurithi mikoba ya mila za Uswega.
Aliwaza sana angewezaje kuwaongoza watu waliomzidi umri. Sauti yake ilikuwa ya
kitoto asingeweza kuongea kwa amri kama baba yake. Angewezaje kuiuliza mizimu
kuleta mvua na amani kwa kijiji chake. Mawazo kama hayo na mengine yalimtafuna
sana kijana Dongwe.
Baada
ya mwaka mmoja kupita, ndipo watu waliruhusiwa kuanua matanga- yaani kumaliza
msiba wa Ntemi wa kijiji. Siku ya mwisho ilikuwa sherehe kubwa sana ambayo
haijawahi tokea kijijini hapo. Ng’ombe walichinjwa mpaka walaji wa chibulanga wakachoka kukinga damu, vinu
vilikesha vikitwanga mpunga na pombe ilikorogwa kwenye mapipa ya kutosha kiasi
cha kuwalevya walevi hata kabla hawajaanza kuitumia. Ngoma kubwa kwa ndogo
zilipigwa mpaka vijiji vya jirani vikajialika kuja kushuhudia nini kikichokuwa
kikifukuta kwa majirani zao.
Wakati sherehe ikiendelea, wazee wa kijiji
walikutana ajili ya kupanga safari ya kwenda kumtawadha Ntemi kijana Dongwe.
Maana sherehe iliyofanywa ilikuwa sherehe ya kuiaga mizimu ya Nchemu na sasa
kijiji ikilikuwa kinaelekea kosa mizimu ya kukiongoza. Hivyo kwa sababu kimila
mizimu ya Nchemu licha ya kuagwa siku ya leo ingeondoka kesho yake majira ya
jioni. Hivyo basi desturi zilihitaji mizimu mipya kukabidhiwa kijiji kutoka kwa
mizimu ya zamani. Kuchelewesha makabidhiano haya ni kuikaribisha mizimu mibaya
ya magonjwa, vifo na mikosi kwa kijiji chao.
Wazee
walikubaliana kwenda kwa tambiko majira ya alfajiri na wangedumu huko kwa muda
wa siku 10 mpaka mizimu itakapompa kibali Ntemi mpya kuingia katika utawala.
Wazee waliandaa vyakula na wanyama kwa ajili ya chakula chao na kwa ajili ya
tambiko kubwa la siku ya mwisho. Walitawanyika wakikubaliana wangekutana
nyumbani hapo kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea msitu wa matambiko.
Wanakijiji wengine waliendelea na sherehe wakila na kunywa na kucheza ngoma kwa
furaha usiku kucha.
Alfajiri
kabla ya jogoo kuwika wazee wa kijiji na wasaidizi wa Ntemi wakapakia vyakula
vyao migongoni mwa punda, na wengine wakatangulia na mifugo iliyochaguliwa kwa
ajili ya tambiko na nyama. Safari ya kwenda katika msitu wa tambiko ikaanza.
Wazee na vijana wote walitembea kwa haraka kwa miguu yao, Dongwe pekee ndiye
aliyebebwa kwenye kiti kilichobebwa juu na walinzi wa Ntemi. Hofu kubwa njiani
ilikuwa ni kwa kiumbe bundi kulia usiku ule. Kwa mila zao kama bundi angelia tu
safari ilikuwa inaharishwa, maana mlio wa bundi ni uchuro, na sherehe kule
kijijini inangenda kuanza upya ili mizimu isiondoke.
Kwa
bahati njema ndege bundi wenye uchuro mwingi walikuwa watulivu mpaka msafara
ukafika katika msitu mnene wenye uvuli wa kiza kinene. Hakukuwa na mtu
aliyediriki kupita au kukata kuni katika msitu huu. Msafara huu tu ulioingia
sasa nywele zao za visogoni zilikuwa zimesimama kwa hofu kuu. Kiongozi wa wazee
aliomba vijana walete kondoo na akachinjwa chini ya mti mkubwa, ambao ulikuwa
unatisha sana, kama ishara ya Amani.
Kijana
huyu alifanyiwa sherehe ya kurithi mikoba hiyo ambayo ilifanywa kwa siku 10
mfululizo, msitu wa tambiko pia ulikuwa ni msitu wenye wanyama wakali kama vile
nyoka wenye sumu kali koboko, chatu,
simba, fisi, chui na kadhalika. Licha ya wanyama hawa hatarishi kwa maisha ya
Dongwe na wengine, sherehe hizi pia zilitakiwa zifanyike usiku wa kiza totoro
huku wahusika wakiwa wamevua nguo zote na kufumba macho yao huku muhusika peke
yake ndiye aliye kuwa na idhini ya kufumbua mambo yake.
Koboko
aliwika kama jogoo kila ilipokaribia alfarijiri, fisi walikuwa wakisikika
wakicheka kila baada ya jua kuzama na miungurumo ya simba ilikuwa haina muda maalumu.
Kijana Dongwe alijuta kuzaliwa kwani alikuwa na hofu kubwa juu ya sauti za
kutisha za wanyama hao na alijionea mambo mengi makubwa ambayo hakuweza
kuyawaza wala kuyafikiria huko porini. Baada ya siku tatu polini huku chakula
chao kikuu kikiwa ugali na nyama alijikuta akiwa mtu mwenye mawazo mengi sana.
Siku
zilikuwa zinaenda polepole mno kwa akili ya kijana Dongwe alitamani azisogeze
mbele ili atoke kwenye lile balaa lakini wapi, masaa yalikuwa kumi na mbili
mchana na usiku hali kadhalika. Siku ya tano baba yake alimtokea kwenye jozi za
usiku huku akimpa moyo wa ushujaa na ujasiri. Alimuhakikishia kuwa vitu vyote
vingenda salama maana yeye ndiye aliyewakemea bundi kuwika usiku wa safari yao
kuja kwenye tambiko. Dongwe alijikuta akipata ujasiri mkubwa na kujikuta mwenye
furaha na nguvu japo urithi huu hakuupenda kabisa katika maisha yake alijiapiza
moyoni mwake kuusaliti na kutoa elimu pale atakapokua mtu mzima kwani
hakufurahishwa na mambo aliyojionea msituni.
Siku
ya kumi ilipowadia ngoma zilianza kupigwa kwa nguvu huku kiongozi wa wazee
akinyunyuzia damu ya kondoo kwenye mti wa tambiko kwa kutumia mkia wa simba.
Dongwe akaitwa akawekwa katikati ya wazee akawekewa mikono yote kichwani kama
ishara ya kumbariki. Ngoma zilizidi rindima msituni pale. Dongwe aliombwa
kusogea karibu na mti wa tambiko. Alisimama kwa ujasiri na kwenda kusimama
mbele ya mti wa tambiko.
Radi
zilipiga, ngurumo zikarindima msituni pale. Watu wote wakiwa tupu kama
walivyozaliwa na wamefumba macho yao maana atakayefumbua macho ni lazima apigwe
radi au ang’atwe na koboko. Aliyekuwa anaangalia muda wote huu ni kijana
Dongwe. Mara kuhamaki anamuona koboko akimuangalia usoni huku ulimi ukiwa
unatoka na kurudi tena ndani. Dongwe akajipa ujasiri akamuangalia koboko kwenye
macho yake. ‘‘Macho ya koboko ni mazuri na huwa kama anayarembua hivi lakini
sumu yake inatumia muda mfupi sana samba mwilini na kumuua mtu hata kabla ya
kupatiwa dawa,’’ Dongwe alikumbuka maneno ya mama yake.
Mara
ghafla koboko akatoweka! Dongwe hakuamini macho yake, akayafikicha kwa mikono
yake kuangalia vizuri, patupu! Wakati akihamaki mwanga mkali wa radi ukamulika
miguuni kwake. Wakati bado akihamaki na kubaha ikatokea fimbo pale ulipomulika
mwanga wa radi. Sauti nzito ya kuamrisha ikasikika ikimwambia, ‘‘Solaga’’ bila ubishi akainama na kwa
kutumia mikono miwili akaiokota ile fimbo. Alipomaliza tu kuiokota ile fimbo
akaanguka chini, puuu. Ngoma zikaongeza mlio wake radi na ngurumo vikazidi kwa
muda. Dongwe akawa akitapatapa pale chini huku povu jeupe likimtoka mdomoni.
Baada
ya muda kama masaa matatu, Dongwe akaamka. Akaunyoosha mkono wake juu mara radi
na ngurumo vikatulia tuli. Akaonekana kuwa na nguvu za ajabu sana. Akaongea kwa
sauti nzito kama muungurumo wa simba, ‘Nipeni kondoo mzima na kisu.’’
Alipoletelewa akamfunga miguu kwa kamba moja kisha akamtoboa shingo yake na
kuanza kumnyonya damu mpaka kondoo alipokufa.
Dongwe
akawaamuru wote kufumbua macho. Na wote wakafumbua macho. Akaamuru kuni
zisogezwe, kuni zikaletwa mpaka akaamuru kwa mkono kwamba zimetosha. Akanyonya
fimbo yake kwenye kuni mara moto ukawaka. Watu wote wakaogopa sana. Akawaamuru
kuchinja wanyama wote na kumkabidhi damu ambayo aliinywa yote bila kusaza hata
tone.
Dongwe
ameshakuwa Ntemi kamili sasa akamuoka kondoo mmoja na akamla mpaka
alipommaliza. Akawaamuru wazee kula haraka hara na wakatii. Ntemi Dongwe
akasema haya mvua njoo na unyeshe haswa mpaka tutakapofika nyumbani. Ghafla
mvua kubwa isiyo na ngurumo wala upepo ikaanza kunyesha. Wazee wakabaki
wakishangaa lakini Ntemi Dongwe akatoa amri kwa sauti ya simba, ‘‘Tujagi baghosha.’’ Wazee kwa vijana
wakawa wakitetema tu mbele zake. Safari ya kurudi kijijini ikaanza huku Dongwe
akibebwa juu na ngoma zikilia kwa sauti ya juu Zaidi.
HADITHI 2: KASHINDYE MKAUSHA MAJI.
Wananchi
wa kijiji cha Kanyaga walikuwa ni kati ya wanakijiji walioonewa wivu sana wa
wanavijiji wengine waliowazungukuka kwa sababu ya Amani, upendo na furaha kati
yao. Walikuwa sio watu wa kutaka makuu, walikuwa wakitafuta Amani hata na
vijiji vya jirani ili waweze kuishi vyema. Kitu ambocho kinaleta furaha kuna
wakati pia kinaweza leta huzuni kwa kiwango sawa na furaha mpaka
kikakuchanganya.
Hata
hivyo watu wa kijiji cha Kanyaga walikuwa na mila na desturi zao
walizozishikilia kweli kweli bila kufanya jaribio lolote la kuzipindisha.
Watoto waliokuwa wakizaliwa kwa kutanguliza miguu au makalio, Makashindye, na wale waliokuwa
wakisababisha wazazi wao kufariki wakati wa kujifungua walikuwa ni mikosi kwa
familia na kijiji kizima. Mosi walikuwa wakiaminika kuwa wanakausha visima na
mabwawa ya maji ya kijiji. Pili walikuwa wakisemekana kuzuia maendeleo na
mafanikio kwa kila kinachofanyika pale kijijini.
Ilitokea
mwaka mmoja wakati wa utawala wa Nchemu. Kulikuwa na shida kubwa sana ya maji
kijijini Kanyaga na vijiji vya jirani. Kwa sababu kijiji cha kanyaga kilikuwa
bondeni basi vijiji vingine vilikuwa vikileta zawadi ya mazao na mifugo kwa
ajili ya kupewa maji ya matumizi yao wenyewe na mifugo yao. Ilifika kipindi
maji yakawa yanapungua kwa kasi sana. Kati ya mabwawa matano ya maji yaliyokuwa
yakitegemewa na kijiji kizima yalikauka na kubakiwa na bwawa moja tu tena lenye
maji machafu.
Wazee
wakiongozwa na Ntemi Nchemu wakaenda kwa ajili ya tambiko ili kukinusuru kijiji
chao na vijiji vya jirani pia kutokana na shida ya maji. Baada ya tambiko
mizimu ililaumu sana wanakijiji kuendelea kukaa na mtu anayerudisha nyuma
mafanikio ya kijiji na juhudi za mizimu kukineemesha kijiji. Mizimu ilidai kuwa
kuna kashindye anayekausha maji kila
akienda kuchota ndoo moja anaondoka na mapipa Zaidi ya hamsini ambayo mizimu
yake huenda kuyamwaga jangwani. Kazi ikatolewa ya kumtafuta kahindye miongoni mwa wanakijiji wa
kijiji cha Kanyaga.
Baragumu
kubwa iliyotengenezwa kwa pembe la nyati likapulizwa ili kuwakusanya watu chini
ya mwembe mkubwa likalia. Na lamgambo likilia ujue kuna jambo. Watu wote
wakakusanyika na kuwa watulivu kusikia kile walichoitiwa. Wengi alijua ni suala
la maji ila hawakujua maji yangeweza kuwa na matokeo ya kushangaza hivi. Ntemi
alisimama na kuwaeleza wanakijiji kuwa kuna kashindye
na ajitokeze maaa ndiye chanzo cha tatizo kubwa la maji pale kijijini. Kwa
alivyofura mfalme kila mtu alijua kifuatacho ni kifo. Hivyo hakuna
aliyejitokeza.
Mpango
wa kuongezwa kwa kina cha bwawa ukatangazwa ukiwa na lengo la kumpata kashindye. Basi vijana wa kiume wakavua
fulana zao wakabaki vifua wazi wakaanza kuchimba kuongeza kina cha bwawa.
Walipoyakaribia maji wakatolewa vijana wote akawa anaingia mmoja baada ya
mmoja. Alipoingia kashindye mambo
yakamchachia kila akichimba maji yanakimbilia chini. Wenzake walichimba mpaka
wakayakuta maji alipoanza yeye maji yote yakakimbilia chini Zaidi. Chimba,
chimba, chimba na wewe, wapi! Kashindye
akawekwa chini ya uangalizi maalumu nyumbani kwa kiongozi wa sungu sungu wa
kijiji.
Vijana
wengine wakaendelea kuchimba ili kuongeza kina cha bwawa. Maji yalipatikana kwa
wingi sana na watu wakaruhusiwa kuchota maji yale wala hayakupungua tena.
Lakini kila mmoja akawa akishangaa kwa nini mwanakijiji mwenzao aliyeitwa
Marando leo ameonekana kuwa ni kikwazo kwa kijiji kizima. Wote walikuwa
wakimfahamu sana na hata nyumbani kwa wazizi wake palikuwa panajulikana.
Familia yao hawajawahi kupatikana na tuhuma za uchawi au wizi hata siku moja.
‘‘Leo umekuchaje kwa Marando jamani?’’ Walishangaa sana.
Wazee
walikutana kwa ajili ya kutafuta watu ambao wangeenda timiza adhima ya mizimu
ya kumuua kashindye katika msitu wa
tambiko tena kikundi hiki kilipendekezwa kuwa kiwe ni kikundi endelevu kwa
ajili ya kutekeleza adhabu ya kifo kwa makashindye,
wanaosababisha vifo vya wazazi wao na wachawi wa kijiji kile. Sangijo, Mtupa,
na Kitinde ndio waliochaguliwa kuwa kikundi cha kukomesha mikosi pale kijijini
kwa sababu ya ukubwa wa miili yao hivyo wasingeshindwa kitu.
Vijana
hawa waliitwa kwenye baraza la wazee na kupewa maelekezo na kwamba baada ya
kufanya tukio lile wazee wangewafanyia matambiko ili wasijedhurika. Maana
inaaminika mtu akitoa uhai wa mtu mwingine basi lile jinamizi la marehemu
linamuwinda muhusika mpaka litakapolipiza kisasi cha roho ndipo linapumzika au
hata kuendelea kutoa roho zingine za wanafamilia mmoja baada ya mwingine.
Vijana hawa watatu licha ya kwamba walikuwa na misuli na maumbo makubwa ya
miilii yao lakini mioyo yao ilikuwa na uoga mno. Ila hawakukataa wito wa wazee.
Walipanga
jioni ile wakamfunge kwenye gunia kubwa ili asiwatambue. Maana kiongozi wa
sungu sungu alikuwa amemweka Marando kwenye chumba chenye kiza sana, hivyo
Marando hakuwa akijua kuwa nje ni usiku au mchana. Walitafuta gunia kubwa la
katani, Kamba nzuri za katani, mapanga matatu yaliyonolewa vizuri na shoka
moja. Kama mtu angekutana nao alfajiri angejua wanaenda kuchinja ng’ombe
mahali. Kwa ukimya na huzuni kubwa walikula chakula chao cha jioni ili wasije
wakazidiwa nguvu wakati wa kutimiza maelekezo waliyopewa na wazee wa kijiji.
Vijana
kwa ujasiri wakakiingia chumba alichokuwamo Marando. ‘‘We ni nani?’’ Marando
aliuliza kwa hofu. Akastushwa na ngwara aliyopigwa akaanguka kama gunia la
viazi vibovu. Hajakaa sawa akajikuta ndani ya gunia, akanyanyuliwa mzega mzega.
Hofu ikamjaa Marando akaangua kilio kikuu lakini kila aliyesikia kilio chake
alifunga mlango ili nae aangue kilio chake akiwa ndani ya nyumba yake. Kila mtu
alimpenda Marando pale kijijini lakini amekuwa akitembea na bahati mbaya ndio
maana hata wasichana walikuwa wakikataa kuolewa nae bila sababu za msingi. Kwa
hiyo watu walilia kwa sababu ya kumpoteza mtu ambaye walikuwa wakikusudia labda
angepata furaha baadae lakini wapi.
Kilio
cha Marando kikageuka kuwa mayowe yaliyozidiwa nguvu na unene wa misitu
waliyokuwa wakiiipitia. Wazazi wa Marando walijiondokea kijijini hapo siku ile
ile mototo wao mpendwa wa kiume aliposemwa kuwa ni mkosi wa kijiji kizima.
Hawakuweza kuvumilia mototo wao aliyeyekuwa na machungu ya kukataliwa na
wasichana wa kijijini hapo eti leo anakuwa mkosi wa kijiji na anatakiwa
kuuuwawa bila maelelezo yanayojitosheleza. Hata hivyo miungu huwa haihojiwi
ndio maana waliamua kuhama kijiji cha Kanyaga.
Walipokaribia
msitu wa tambiko simba akaunguruma mara tatu mfululizo. Marando akanyamaza na
kujikuta anajisaidia haja dogo. Vijana wale watatu baada ya kuona
wanalowanishwa na mkojo tena wa mtu mzima wakamshusha chini kimya kimya,
wakaoneshana ishara kwamba Mtupa ampige shoka la shingo na warudi ili wasije
wakadhuriwa na simba. Mtupa hakuwa mbishi akachukua shoka akalinyanyua wima juu
ili alishushe na kutenganisha kichwa na kiwiliwili cha rafiki yake wa tangu
utotoni.
Shoka
likagoma kushuka, machozi yakaanza kumtoka wenzake wakamuonesha ishara ashushe
shoka inapoonekana kuwa ni shingo. Mtupa akaangua kilio kwa nguvu akasema
‘‘siwezi kufanya hivi sitaweza kuishi kwa Amani abadani.’’ Alipomaliza kuongea
tu. Marando akaifahamu sauti ya rafiki yake kipenzi. Marando akamwambia,
‘‘Mtupa rafiki yangu naomba unisaidie, unanifahamu mimi na matatizo yangu
naomba uniokoe hapa tu.’’ Sangijo na Kitinde nao wakaanza kulia kwa uchungu mno
pamoja na rafiki yao.
Wakajikuta
wanamfungulia na kumwambia ‘tunaokoa maisha yako ila maisha yetu yatakuwa
hatarini mpaka kufa kwetu endapo utaonekana na mwanakijiji yeyote wa Kanyaga.’
Wakamuomba akimbimbie aende kijiji cha mbali kwa ajili ya kujitafutia maisha
huko. Marando hakusubiri neno lingine alifukua mbio kama anakimbizana na
malaika wa kifo.
Mtupa,
Sangijo na Kitinde wakarudi kijijini wakiwa na huzuni katika nyuso zao. Wazee
wakawapa kila mmoja ng’ombe ishirini na mbuzi kumi. Na kuwaahidi kama wangeanza
kujisikia hatia au mikosi basi waombe tambiko la wazee. Kijiji kizima kilijaa
na huzuni isiyosemekana kwa muda usiojulikana. Hata wale wasichana waliomkataa
Marando walimuonea huruma sana. Huzuni ziliisha kwenye nyuso za watu lakini
zikabakia kwenye mioyo yao
HADITHI 3: MALKIA KASHINDYE
Utawala
wa Ntemi Dongwe ulikuwa utawala haswa. Kila mtu aliweza kusema Dongwe alikuwa
na mizimu yenye nguvu na makini kuliko watangulizi wake waliomtangulia yaani
baba yake na babu yake. Ntemi Dongwe kijana mdogo mwenye mipango mikubwa na
madhubuti isiyotiliwa hata lepe la wasiwasi kwa wanakijiji wa Kanyaga. Baaadhi
ya wakazi wa vijiji vya jirani walikuja kuomba hifadhi au makazi ya kudumu katika
kijiji cha Kanyaga kwa sababu ya chuki na uhasama wa wao kwa wao au na viongozi
wao. Wanakijiji hata wa vijiji vya jirani walimwamini na kumpenda sana Ntemi
wao Dongwe.
Dongwe
alikuwa masikioni, midomoni na mioyoni mwa wanakijiji wote. Lilikuwa sio jambo
la kushagaza kuona raia wakienda Ikulu,
nyumabani kwa Ntemi kupeleka shina la muhogo lililozaa isivyokawaida au kondoo,
mbuzi au ng’ombe aliyezaa mapacha alikuwa yeye na ndama wake ni mali ya Ntemi.
Na watu walikuwa wakienda kufanya matambiko kwenye miungu yao ya familia kwa
ajili ya mifugo yao kuzaa mapacha ili waipeleke kwa Ntemi. Ilikuwa ni sifa kwa
kijiji kizima kupeleka kitu kilichotofauti na vingine kwa Ntemi.
Kwa
bahati mbaya Ntemi alipofikisha umri wa miaka 20 akaanza kuugua maradhi
yasiyojulikana. Akaitwa mganga mkuu anayeaminiwa na kijiji kizima ili aweze
kuokoa maisha ya Ntemi huyu aliyependwa na kijiji kizima. Wanakijiji wakawa
wakimuombea Ntemi wao kwa miungu yao ili aweze pata nafuu na kuwaongoza kama
ilivyokuwa kwa miaka yake iliyopita. Mganga tegemeo la kijiji kizima baada ya
matibabu ya mlima wa mizizi kuonekana kutofua dafu akatangaza kushindwa.
Basi
watu wakawa wakijaribu kila dawa waliyoiota labda ingempa mfalme Amani lakini
haikuwa hivyo. Ntemi alikuwa akinukia shubiri wakati mmoja na wakati mwingine
angenukia mdalasini, iriki na karafuu lakini bila nafuu. Wakawatangazia
wanakijiji wa vijiji jirani nao kwa upendo na Ntemi huyu walikuja na mizizi ya
meno, mikaa ya migomba na nini sijui lakini hali ya mfalme ikawa mbaya Zaidi.
Waganga wakatoa tofauti zao wakakaa kikao kwa ajili ya kumuokoa mfalme lakini
bila mafanikio.
Dau
likatangazwa kwa vijiji vya mbali Zaidi kama kawaida ya waganga wakatandika
punda wao wakawabebesha mizigo ya mizizi, mafuvu ya fisi na vyote wanavyovijua
waganga. Lakini mfalme hakutoa hata jasho la ahueni. Watu wakakata tamaa
wakaweka dawa zao pembeni na kuanza kufanya usihiri kuzungunga ikulu lakini
wapi nafuu ya Ntemi?!
Habari
za kuugua kwa mfalme zikayafikia masikio ya Marando, japo alikuwa mzee wa umri
lakini hakuwahi kusahau kuwa moyo wake ulifurahi kuishi katika kijiji cha
Kanyaga. Marando alikuwa na binti aliyeitwa Maua, Maua alikuuwa maua kweli
mrembo sana mwenye umri wa miaka 18 hivi. Aliposikia ugonjwa wa Ntemi akampasha
habari binti yake kuwa wakati wa kurudi kuishi katika kijiji cha Kanyaga kwa
furaha na Amani umewadia. Maua alihamaki wangerudije na wakati walitakiwa
kuuwawa?
Marando
akamwambia dawa ya mfalme ninayo mimi na sitavumilia kuona Ntemi mwenye moyo
mzuri kama yule anapoteza maisha. Maua akakubaliana na baba yake na kwenda
Kijijini Kanyaga. Kwa sababu watu walikuwa wamekwisha wasahau hivyo hata
hawakutaka kwenda kwa kujificha walienda mchana kweupee. Waliposema wana dawa
ya kumtibu mfalme basi wakapewa walinzi kuwasindikiza kwenda kwa mfalme. Moja
kati ya walinzi wale alikuwepo Mtupa rafiki kipenzi wa Marando. Marando
alimtambua ila hakumwambia neno lolote.
Walifika
kwa Ntemi na kabla ya matibabu kuanza, Marando alimuuliza Ntemi kwa sauti ya
kinyenyekevu kuwa alikuwa anaumwa nini. Walinzi wakamwambia Marando, ‘‘Mganga
hilo swali bwana Ntemi huwa hapendwi kuulizwa, we mtibu tu kama una dawa kweli
atapona atapona.’’ Maranda akawahakikishia kuwa dawa yake ipo kwenye maongezi
na kwamba kama mfalme angeongea tu yeye dawa yake ingeanza kazi.
Siku
ya kwanza ilipita mfalme hakuongea neno. Alikuwa anajigeuza tu huku na kule na
kuguna kana kwamba ana maumivu makali sana. Alikuwa akikaa muda anashusha pumzi
kwa nguvu kama mtu anaetaka kata roho. Siku sita mganga huyu alikuwa tu
chumbani mule kwa Ntemi akisubiri kusikia sauti ya Ntemi. Waganga wengine Ntemi
alikuwa anawaoneshea ishara ya kuwafukuza pale tu walipomtaka aongee lakini
haikuwa hivi kwa mganga Marando na binti yake Maua. Kadiri walivyozidi kukaa
ndivyo mfalme alivyokuwa akijisikia Amani na kula chakula chake vizuri kuliko
ilivyokuwa hapo awali.
Walinzi
walikuwa wakishangaa kumuona mganga huyu ambaye hakuharibu msitu kwa kuleta
tela la mitishamba kama wenzake. Wakawa wakisemezana kuwa kweli duniani kuna
waganga yani anataka Ntemi amjibu tu ili aanze kupona. Hili nalo linaweza kuwa
mfano wa ajabu la dunia. Wabeba mikoba, wazee na wanakijiji walihamaki kusikia
kile kinachoendelea kwa Ntemi. Wote wakatamani kumshurutisha Ntemi aongee
lakini Mganga na binti yake waliwaambia kutokumshurutisha maana wangeharibu dawa
yake.
Tatizo
la siku na wiki ni kama una kitu unachosubiria kwa hamasa sana huwa zinaenda
polepole mwendo wa konokono. Watu walikuwa wanaona kesho za jana zikipishana
kwa kasi ya kinyonga bila Ntemi kuongea na mganga wao. Lakini hakuna marefu
yasiyokuwa na ncha, siku moja baada ya chakula cha mchana mfalme akawafukuza
watu wote toka chumbani. Watu wakatoka kwa furaha wakijua kuwa Ntemi wao
amechagua kupona siku ile. Watu wakaenda kusimulia kila kilichokuwa na masikio
na taarifa yao ilikuwa na wasikilizaji wengi mno.
Mfalme
akamwambia Marando, ‘‘mimi sijui naumwa nini! Ila nilipowaona nyinyi nimeanza
kupata nafuu.
‘‘Huwezi
kuwa hauumwi kitu mtukufu Ntemi, kuna kitu kinakudhoofisha’’ alijibu Marando.
‘‘Kiukweli
nilianza tu kujisikia moyo unakuwa mzito mpaka nashindwa kufanya kazi zangu.’’
Ntemi alijaribu kujieleza.
Baada
ya udadisi mkubwa Marando akamwambia Ntemi kuwa ameugundua ugonjwa wake na siku
iliyokuwa inafuata wangeenda kuchimba dawa wakiwa watatu tu. Hawakutaka mtu
mwingine awafuate maana wangeenda kuharibu dawa ya Ntemi. Watu walikubali na
Ntemi pia alikubaliana na ombi lile.
Mara
baada ya kifungua kinywa asubuhi iliyofuata basi Ntemi, Marando na Maua
wakaongozana kuelekea msituni, Ntemi akiwa katikati na Marando akiongoza njia
huku Maua akiwa nyuma na amebeba jembe mkononi mwake. Walitembea kimya kimya
wakimtaka Ntemi azidi kutafakari kuhusiana na kitu chochote kinachomsumbua ili
wamchimbie dawa huko waendako. Walipofika njia panda ya kwenda msitu wa tambiko
na ile inayoenda kijijini kwa Marando wakasimama.
Mara
Marando akamgeukia mfalme na kumwambia mfalme akumbuke kuna kitu alilowahi
kukifanya njia panda. Mfalme akamwomba iwe siri kwa sababu ni siri aliyoitunza
maisha yake yote. Ntemi akasema nakumbuka baba yangu alitoa amri kwa msichana
kashindye aliyekuwa na wiki moja tu kuja kutupwa msitu wa tambiko lakini mimi
niliwafuatilia nyuma wale wauaji na kumchukua motto pale walipokuwa wamemuweka
ili ajifie au aliwe na wanyama wakali.
Baada
ya kumchukua mototo yule Ntemi hakujua ampeleke wapi mara kwa nasibu akapita
mwanaume wa makamu akielekea kijiji cha mbali kwa njia inayoelekea kijijini
kwenu. Ntemi akamuomba yule mwanaume aende kumtunza yule binti na akikua
ajitahidi kumleta japo amuone tu kwa siri. Basi yule mwanaume alikuwa mkarimu
sana na kuniambia angefanya vile alivyoombwa na Ntemi Dongwe. Lakini miaka
imepita mingi bila Ntemi kusikia taarifa ya yule binti hivyo alidhani huenda
aliukabidhi mzimu na ulienda kumdhuru yule binti.
Ntemi
akasimulia namna ambavyo Marando, kashindye wa kwanza alivyoenda kuchinjwa bila
huruma katika msitu wa tambiko. Huzuni ile aliapa kutoiruhusu itokee tena
maishani mwake na ndio maana alipoona wanaenda kumtupa yule binti wa wiki moja
alipanga kumsaidia licha ya kwamba hakujua angempeleka wapi. Basi, mfalme akawa
muwazi kwa mganga huyu asiyemfahamu na kumuomba asitoe ile siri yake ya kuugua
ugonjwa usiojulikana.
Marando
na Maua wakajikuta wakibubujikwa na machozi na kuangua vilio kwa pamoja. Ntemi
akahamaki sana na kuuliza kulikoni. Marando akamsimulia kwanza mkasa wake na jinsi
vijana Mtupa, Sangijo na Kitinde walivyoyanusuru maisha yake na pili
akamkumbusha kuwa yeye ndiye aliyemchukua Maua na kwenda kumlea mpaka alipokua.
Marando baada ya kusaidiwa aliamua kuja kulipa fadhira kwa Maua ambaye alipata
taarifa zake kwa wachota maji wa kijiji chake kuwa angetupwa porini na akaamua
kuja kumuokoa. Marando akasema nilijua kama kweli Ntemi angekuwa anakumbuka
fadhira zake mawazo yake yasingemtulia. Ndiyo sababu hakuleta taarifa yoyote ya
Maua kwa Ntemi.
Ntemi
alifurahi sana na kuwaamuru kuwa ile siri iwe miongoni mwao tu. Waliporudi
kijijini Ntemi akawashangaza Marando na Maua baada ya kutangaza kuwa wiki
inayofuata alikuwa anaoa na angemuoa Maua kwani ndiyo dawa yake. Kwa hiyo watu
wakaadhaa sherehe ya harusi ya Ntemi. Watu walikula, walikunywa na walicheza
kwa wiki nzima. Kashindye akawa malkia pasipo na mtu yeyeto kung’amua.
HADITHI YA 4: MAGANGA CHA POMBE
Maganga
ni kijana wa makamu alieishi upande wa magharibi wa kijiji cha Kanyaga. Maganga
licha ya kuwa kijana mdogo aliyekuwa anakadiriwa kuwa na umri wa miaka kama
selathini hivi, alikuwa tayari ameshaoa mitala ya wanawake watano, huku akiwa
na mtoto mmoja. Mke mkubwa wa Maganga alijulikana kwa jina la Kabula au mama
Wande. Mke wa pili aliitwa Nchoji, mke wa tatu aliitwa Milembe, wanne aliitwa
Siha na watano aliitwa Masele.
Maganga
alikuwa kijana mchapa kazi sana aliyeyejishughulisha na kilimo cha mpunga,
mahindi na miwa. Kila mwaka alikuwa na uhakika wa kuvuna magunia mia na hamsini
ya mpunga na magunia mia na ishirini ya mahindi. Kabla hajaoa alikuwa akiuza
mazao yake siku ya gulio na kununua ng’ombe ambao walimsaidia Zaidi kwenye
shughuli za kilimo. Kuna kipindi aliwahi fikisha jozi kumi na nane za Nzagamba, maksai wa kulimia.
Wazazi
wengi walikuwa wakimpigia mfano kijana Maganga kwa vijana wao wavivu na
wasiojishughulisha. Kwa wazazi wengi walitamani sana vijana wao wawe kama
Maganga. Maganga hakujua kwenda kukaa kijiweni kula miwa na kupiga soga kama
vijana wengi wa kijijini pale walivyofanya. Yeye aliamka kabla ya mawio ya jua
na kuelekea shambani au kwenye majaruba yake ya mpunga kwa ajili ya kulima,
kupalilia au kuangalia maendeleo ya mazao yake.
Kusema
ukweli Maganga alikuwa ameliteka hata soko la mazao kijijini pale. Maana yeye
alikuwa akiweka akiba ya mazao yake stoo na kusubiri yakiadimika ndipo aanze
kubadilishana na mifugo. Msimu wa kuvuna mazao ulipofika Maganga ndiye alikuwa
mnunuzi mkuu wa mazao ya wanakijiji wengine. Na wanakijiji walipenda kumuuzia
mazao kwa kuwa hakuwafanyia dhuruma bali aliwalipa kwa kiwango walichokitaka au
kukubaliana.
Shida
huwa hazipigi hodi, hivyo Maganga alikubali kufuatwa hata usiku wa manane kwa
ajili ya kufanya biashara au makubaliano ya kibiashara. Wakati mmoja alipokuwa
hajaoa bado dada mmoja alikuja kugonga mlangoni kwa Maganga usiku wa giza
totoro. Maganga akauliza akiwa ndani kuwa ni nani aliyekuwa akigonga mlangoni.
Sauti ya kike nyororo ilijibu kuwa, ‘‘Ni mimi Kabula.’’ Maganga akafungua
mlango na kumsikiliza mgeni wake akiwa mlangoni bila ya kumkaribisha ndani.
Kabula
alikuwa amekuja kuomba msaada wa tela la ng’ombe linaloendeshwa na jozi moja ya
ngombe ili ampeleke baba yake kwa mganga wa jadi maana alikuwa hoi bin taabani.
Kabula akamwambia alijitahidi kwenda kumuita mganga aje amtibu baba yake
nyumbani kama ilivyokuwa utaratibu wake lakini alimkuta akiwahudumia wangojwa
wengine pale kwake na isingekuwa rahisi kuwatelekeza bila msaada. Hivyo basi
Maganga alimsaidia Kabula kufunga jozi moja ya Nzagamba. Maganga pia alimsaidia Kabula kwenda kumpakia na
kumshusha baba yake kwenye tela maana nyumbani kwa kina Kabula hawakuwa na
kijana wa kiume.
Baada
ya siku mbili kupita Kabula alikuja nyumbani kwa Maganga lakini hakumkuta.
Alipowauliza majirani wakamwambia aliwaaga kwenda kuangalia shamba lake la miwa
ambalo halikuwa mbali. Dada wa watu akamfungia safari na kumfuata mpaka shamba
la miwa la Maganga. Kwa nasibu alimkuta akiwa anafyeka majani yaliyoota katika
njia ya kuliingia shamba lake.
Kabula
alisalimia kwa heshima ijapokuwa kiumri alimzidi Maganga miaka kama mitano hivi.
Lakini mila na desturi za Kanyaga, mwanaume alikuwa anazaliwa akiwa mkubwa
tayari. Hata mama yake Maganga humweshimu Maganga kama baba yake, na hata
alimpa jina la babu yake kwa heshima. Kabula alikuwa amekuja kukopa mbuzi
wawili ili aende akamlipe mganga aliyeyaokoa maisha ya baba yake.
Kabula
alikuwa ni mpishi wa pombe maarufu pale kijijini lakini kipindi cha masika
wateja wake walikuwa wakinywa kwa mkopo wa kuja kulipa baada ya mavuno. Hivyo
hakuwa na kitu chochote cha kumlipa mganga wake wa jadi na kama ilivyojulikana
pale kijijini mizimu huwa haikopwi tiba. Maganga alimwelewa na kumsaidia
kuwapata beberu wawili kama malipo ya mganga wa jadi. Kabula alilengwa lengwa
na machozi ya furaha na kumuaga Maganga huku amepiga magoti ya heshima.
Maganga
alibaki peke yake ndani akimuwaza Kabula kinagaubaga. Alijikuta akimuumba upya
Kabula binti Masanja. Kiukweli alikuwa ni msichana mlimbwende sana, mwenye
heshima na ustaarabu wa hali ya juu. Vijana wengi pale kijijini walimuogopa kwa
sababu alikuwa hapendi mizaha ya hovyo hovyo. Maganga alijikuta anampenda
Kabula ila alikuwa hawezi kuongea na msichana yeyote kuhusu mapenzi na ndoa.
Mawazo ya Kabula yakamletea usingizi mzito na akalala kama pono.
Alishitushwa
toka usingizini na hodi za mfululizo zilizogongwa mlangoni. Kwenda kufungua
mlango akabaha alipokutana na uso wa mviringo wa Kabula. Akamkaribisha ndani
huku akimpokea kikombe kikubwa kilichokuwa kimefunikwa. Alipoingia ndani,
Kabula akaomba radhi kwa kumuamsha Maganga toka usingizini. Akamwambia moyo
ulimsukuma amletee pombe yake kidogo ili aonje. Maganga alikuwa sio mnywaji wa
pombe. Hata kwenye sherehe kubwa alikuwa akitumia togwa tu.
Lakini
zawadi inanguvu ya kubadili maamuzi na mipango ya mtu ya muda mrefu. Wakati
Maganga akiwaza labda amsubiri Kabula aondoke ili akaimwage pombe yake, mvua
kubwa ikaanza kunya kijijini Kanyaga. Kwa sababu Kabula na Maganga walikuwa
hawana mazoea wakajikuta wakikosa cha kuongea. Kabula akachukua kile kikombe
cha pombe na kukikabidhi kwa Maganga kwa magoti ya heshima huku akimwambia,
‘‘Karibu uonje pishi langu sijakuwekea kilevi sana maana najua huwa hupendi
pombe.’’
Yale
magoti na ile sauti nyororo vilifanikiwa kumtoa nyoka pangoni. Kijana Maganga
akapokea kile kikombe akakata mafundo mawili ya uhakika kikombe kikabaki nusu-
nusu ya kujaa au nusu tupu vyote sawa ila inategemeana unamuwazia nini Kabula.
Baada ya kupita dakika kama tano za ukimya, ukimya mzito wa kukata na shoka,
Maganga akaanza kupayuka kwa sauti ya juu. ‘‘Wewe, Kabula ni mzuri sana. Mimi
nataka nikuoe sasa hivi.’’ Maganga akamalizia mafundo yake mawili na
akamsogelea Kabula.
Baada
ya mvua kuisha nao wakawa wamekwisha kabisa na Kabula akaaga kwa heshima na
kuondoka. Ulevi ulikuwa haujamuisha Maganga na Kabula alijua fika ila
akaondoka. Lakini ondoka yake ilikuwa ondoka ya kurudi tena kwa sababu alifunga
mlango kwa nje. Kiza kinene kilitanda na Maganga akiwa anajiongelesha tu mule
ndani kwake. Mara mlango ukafunguliwa, Kabula akaingia akiwa na kapu la
chakula. Maganga akampalamia Kabula lakini Kabula alikuwa mpole na mwenyekusihi
sana kwamba wale chakula kwanza, hivyo Maganga akakubali kula chakula cha
kwenye kapu halafu waangalie uwezekano wa chakula kilichodondokea chini ya
sketi.
Hivyo
ndivyo Kabula alivyoolewa na Maganga au tunaweza kusema, Kabula alivyojioza kwa
Maganga. Maganga akaanaza kuwa mlevi mzuri wa pombe ya mke wake. Alikuwa
anakunywa mara moja kwa siku, akajikuta anaongeza idadi kuwa mbili, tatu mpaka
akawa hawezi ishi kwa lisaa limoja bila ya kunywa pombe. Kabula alimkaa haswa
moyoni na pombe ikapata nafasi yake kichwani. Pombe ikawa ndio kazi na kazi
ikawa ndio pombe. Kuna siku alikunywa pombe mpaka akajinyea uharo palepale
alipoketi.
Mapenzi
huleta watoto kama mizimu ya ugumba haijamkasirikia mwanamke ndivyo
ilivyoaminika pote katika kijiji cha Kanyaga. Kabula akawa mjamzito. Na kwa
bahati mbaya mimba yake ikamwendesha kweli kweli. Akawa hali chakula maana
akila tu anatapika mpaka nyongo. Akawa hafanyi kazi yoyote isipokuwa kulala na
kula udongo, ndimu na maembe machanga. Mlevi aliyepindukia, Maganga akajikuta
katika wakati mgumu sana. Kuishi bila pombe ilikuwa ni mwiko kwake, akaanza
kuitafuta pombe vijiji vya jirani.
Ulevi
wa Maganga ulikuwa mbaya sana, japo sijawahi kuona ulio mzuri, kwani baada ya
kichwa chake kulewa mikono yake ilitaka papasa sehemu za miili ya wanawake
waliokuwepo kirabuni pale. Kuna siku alilewa chakali halafu akaanza kumtomasa
mwanamke aliyekuwa karibu nae. Lilikuwa
kosa la jinai maana mumewe alikuwa nae pale pale kirabuni. Maganga alipigwa
vichwa vya mdomo, makofi na mitama mpaka watu wakamuonea huruma na kumuokoa.
Akarudi nyumbani akiwa amelowana damu kwenye nguo zake zote na uso wake
ulivimba sana hasa maeneo ya mdomoni. Mke wake alipomuona alilia sana. Maganga
aliogeshwa, akakandwa na kubadilishwa nguo.
Asubuhi
yake pombe zilipomtoka alijuta sana akaapa kwa mzimu wa baba yake kuwa
asingelewa tena. Lakini mlevi ni mlevi tu hata kitokee nini. Matukio huwa
hayambadilishi mlevi labda aishiwe kiu ya ulevi wake. Zilipoisha siku mbili,
Maganga akapata hamu ya pombe hadi kichwa kikaanza kumuuma. Akawaza na kupata
sulihisho kuwa angeenda kijiji kingine na hata kuwa mgomvi tena. Baada ya
kujishauri akaondoka nyumbani bila kuaga akaenda kijiji kingine kutafuta pombe.
Alipofika kule akaanza kujitapa juu ya mafanikio yake. Na wengi wao walikuwa
wakimfahamu vizuri.
Baada
kuwa wamekunywa mpaka karibia usiku wa manane, mzee mmoja alimkaribisha kwake
ili apumzike kwa usiku ule. Maganga alikubali wito kumfuata mzee yule mpaka
nyumbani kwake. Mwenyeji wake alimuonesha chumba cha kulala na kumuwashia
kibatari. Maganga aliletewa chakula na binti wa pale nyumbani. Binti alikuwa
mlimbwende hasa, matatizo akawa anameza tu funda baada ya funda la mate.
Alikula chakula huku binti amepiga magoti pembeni yake. Uzalendo ukamshinda,
akamuuliza jina lake ambalo hakuwa hata na kazi nalo. Binti alimwambia kuwa
aliitwa Nchoji.
Maganga
aliacha kula na kuanza kukichungunguza kifua cha Nchoji. Kipimo cha uvumilivu
kilikuwa kimefika kikomo kwa Maganga. Akasimama akaenda funga mlango halafu
akamwambia, binti nataka uwe mke wangu. Twende wote Kanyaga tukale mali zangu
maana ni nyingi mno siwezi zimaliza peke yangu. Ila ninaombi moja tu,
ukinikubalia tunaenda wote Kanyaga. Ombi lenyewe hata halikuwa ombi bali
lilikuwa takwa maana Nchoji alikuwa hajaelewa bado nini kikiendelea mlevi akawa
ameshafika kifuani na baada ya muda akamlaza kwenye ngozi iliyokaribu nae na
kujikaribisha kwa huduma, ambayo muombaji alikuwa hajakubali wala kukataa.
Nchoji
alishindwa kupiga kelele licha ya maumivu aliyokuwa akiyapata. Hakujua kwa nini
ila umasikini wa nyumbani kwao ulichangia yeye kukaa kimya ili kwa machungu
haya ya muda aende kufurahia maisha huko Kanyaga. Asingeweza kukimbia maana
baada ya yote alitakiwa alale na mgeni japo kwenye ngozi tofauti. Wakati mawazo
yakimzunguka kichwani Nchoji, mlevi alishuka na kulala pembeni yake huku
akimtomasa tomasa sehemu zake za kifuani.
Asubuhi
mzee mwenye mji na Maganga walipangiana mahali ya ng’ombe ishirini na wangeenda
kuchagua wenyewe kwenye zizi la Maganga kijijini Kanyaga. Msafara ulijiandaa,
Nchoji hakuwa na vitu vingi vya kubeba sana sana alijibeba mwenyewe tu, mama
yake alipiga vigeregere vya furaha na vya kumuaga binti yake. Wanakijiji
walisemezana kuwa Nchoji ameukata. Amewaachia shida zao pale kijijini kwao.
Msafara uliongozwa na mwenyeji Maganga na kufuatiwa na Nchoji, Baba yake
Nchoji, Mjomba wake Nchoji na walevi wawili. Safari ilikuwa ndefu lakini
walifika na kumkuta Kabula kajilaza hoi kwenye kivuli cha mwembe ulio karibu na
nyumba.
Maganga
alimuita mkewe pembeni na kumwambia kuwa amemletea msaidizi pale nyumbani.
Japokuwa Kabula hakupenda kuolewa mke mwenza mapema vile ila aliufyata mkia.
Nchoji akakabidhiwa jiko, vijana wakachinja mbuzi na sherehe ndogo ikafanywa na
baadae baba mkwe akabagua ng’ombe wake toka zizini na kuanza safari ya kurudi
kijijini kwake. Nchoji alipewa chumba chake cha kujitegemea na Maganga akawa
akilala au kujipumzisha kwenye chumba cha Nchoji tu. Wivu ulimshika Kabula
lakini hakuwa na uwezo wa kufanya chochote.
Maganga
alioa wanawake watatu wengine kwa mtindo huu huu kama alioutumia kwa Nchoji.
Alipoenda kulewa tena mzee mmoja alikuwa akimchangamkia na kumywesha pombe
nyingi na baadae kumkaribisha nyumbani. Wake walioongeza ukubwa wa familia ya
bwana Maganga ni Milembe, Siha na Masele. Wake walioolewa baada ya Kabula wote
walikuwa wadogo wadogo wenye umri kati ya miaka kumi na tatu hadi kumi na saba.
Hivyo wote walizidiwa kiumri na Kabula mbali sana.
Siku
moja Kabula akawashauri wake wenza waanze kupika pombe pale kwao maana mume wao
angeoa kijiji kizima kwa tabia yake. Wakafanikiwa kumdhibiti kwa pombe maana
kila akikohoa aliletewa pombe na moja kati ya wake zake. Aliona maisha
yamemnyookea maana aliiishi kama mfalme pale nyumbani. Alikuwa kiletewa vyakula
muda wote mpaka vingine akawa akionja tonge mbili ili kumfurahisha mke wake
aliyeleta chakula kwa zamu yake.
Mbinu
ya wake zake na Maganga ilizaa matunda kwani ilipita miezi sita bila mume wao
kuongeza mke mwingine au kwenda kulewa kijiji cha jirani. Kwa bahati mbaya sana
mbinu yao iliishiwa nguvu mara pale wote walipojigundua ni wajawazito. Kila
mmoja akawa akitafuta udogo, ndimu au ukwaju ili kuondoa kichefuchefu mdomoni
mwake. Maganga akawa huru tena kutembelea virabu vya pombe vya vijiji vya
jirani.
Siku
moja baada ya kunywa na kulewa haswa hadi akalala na kutoa haja ndogo na kubwa
pale pale akakosa mfadhili wa kwenda nae nyumbani. Alikuja kuzinduka saa saba
za usiku na kuanza safari ya kurejea nyumbani. Kwa bahati mbaya alipofika
msituni akajikwaa kwenye kisiki na kuanguka. Alishindwa kuamka kwa sababu ya
uchovu aliokuwa nao. Akaazimia alale kidogo akiamka ataendelea na safari.
Akalala fofofo.
Kiumbe
chatu akiwa kwenye mawindo yake akitafuata kitoweo. Chatu alijiona mwenye
ngekewa baada ya kukutana na kitoweo kimejilaza tena kando ya njia. Chatu
akaanza kuuramba mwili wa Maganga ili ateleze vizuri kuingia tumboni mwake.
Chatu akaupakaza mate mwili mzima wa Maganga. Akaanza kummeza kuanzia miguuni.
Kwa nasibu, Maganga alilala huku ametanua msamba. Hivyo chatu aliumeza mguu
mmoja tu wa Maganaga na kushindwa kuendelea kwa sababu mguu mwingine ulikuwa
mbali, hivyo akatulia.
Maganga
fahamu zilipomjia kwenye usingizi wake akajisijia joto kwenye mguu wa kushoto.
Akajisemea kimoyomoyo, ‘inamaana leo mama wande ameamua kunifunika mguu mmoja
tu.?’’ Basi akaamua kuulazimisha na mguu wa kulia kinywani mwa chatu na
kujisokomeza mwili mzima mdomoni mwa chatu. Na chatu hakufanya ajizi, akammeza.
Maganga akamezwa na chatu. Ndio maana hadi leo wanakijiji wa Kanyaga hawaendi
kunywa pombe vijiji vya jirani.
HADITHI YA 5: MAKOYE, MCHAPA KAZI
MWENYE BAHATI YA KIFO
Zamani
za utawala wa Ntemi Doi, kijiji cha Kanyaga kilikuwa kikipigana vita sana na
vijiji vya jirani. Vita hizi zilikuwa zikitokana na baadhi ya vijiji kutafuta
mateka wa vita ambao wangewatumia kwa ajili ya shughuli za kilimo ili kuongeza
uzalishaji kijijini mwao. Vijiji vilivyokuwa vikipenda kuja kwa mapigano ya
vita vilikuwa ni kijiji cha Ikindika na kijiji cha Nyahanga.
Siku
moja kijiji cha Ikindika kilivizia mnamo usiku wa manane na kuchoma nyumba
nyingi za kijiji cha Kanyaga. Wanakijiji wa Kanyaga walikimbia hovyo hovyo na
kuuawa kama kuku. Wanaume wenye misuli walichukuliwa pamoja na wanawake
walimbwende wa kijiji. Mifugo iliyonona pia yote ilibebwa na maharamia wa
kijiji cha Ikindika. Kijiji kilibakia na wazee, watoto na wanawake. Ntemi Doi
na walinzi wake walikimbilia porini kujificha.
Moja
kati ya vijana waliokamatwa alikuwa ni Makoye. Makoye alikuwa mchapa kazi sana.
Alikuwa na ng’ombe wake aliowatenga kwenye makundi mawili kila kundi ng’ombe
mia tano. Alikuwa na mbuzi wasio na idadi na kuku aina ya kuchi ambao kila mtu
alikuwa akiwatamani pale kijijini. Maharamia wa kijiji cha Ikindika walibeba
mali nyingi za kijana Makoye bila kujua. Kweli mali inamfuata mwenye nayo,
waliobaki kijijini pale walijisemea.
Njiani
kote Makoye alikuwa akiwaza kuhusiana na kupoteza mali zake zote kwa pamoja na
pigo baya zaidi ni yeye kuchukuliwa kuwa mtumwa. Makoye alijikokota kuelekea
utumwani asikokujua na mbaya zaidi alikuwa amemposa binti mlimbwende wa kijiji
kizima, Masele binti mfalme. Sherehe yao ya harusi ilibakiza siku tatu tu
ifanyike hata hivyo maandalizi yalikuwa yakifanywa kwa umakini wa juu mno. Hata
kabla ya usiku huu wazee walikutana kwa ajili ya kupanga ratiba ya upishi siku
ya harusi.
Lakini
vita huwa haina macho, yenyewe huharibu mipango ya watu na hata kukatisha
maisha yao. Wakati wakitembea kuelekea kijiji cha Ikindika kilichopo umbali wa
maili kumi na nane hivi toka Kanyaga, jua lilianza kuchomoza hivyo watu
wakaanza kutambuana kwa sura. Makoye kutupa jicho huku na kule akamuona kipenzi
chake Masele binti mfalme ameshikiliwa mkono na ambaye alikuwa kiongozi wa
jeshi la jadi la Ikindika. Alitamani kutabasamu lakini hakuweza kwani kipenzi
cha moyo wake naye alikuwa ametaifishwa.
Baada
ya safari ndefu huku Makoye akitamani kufa kuliko kuendelea kuyaona anayoyaona,
aliamua kujiangusha chini makusudi. Walinzi wakatumwa kumuamsha, akajilegeza
kweli kweli ili wamuache au wamuue. Maana ilikuwa inasemekana jeshi la jadi la
ikindika likiwateka wanyonge na waliochoka walikuwa wakiuawa au kuachwa wajifie
kwa njaa na uchovu. Lakini haikuwa hivyo kwa Makoye, kamanda wa jeshi aliamuru
apewe maji na chakula maana alisema huyo angeenda kufanya kasi kwa mfalme wao.
Maneno
yake yalimtia nguvu kidogo Makoye lakini alitamani amuombee na Masele binti
Ntemi aende nae kwa mfalme, lakini alikuwa mateka na huenda mazungumzo zaidi
yangesababisha kugundua mahusiano yao na mbinu zake. Hivyo alikaa kimyaa kama
hajui chochote. Safari ilikuwa inaonesha matumaini kwani waliona nyumba
zilizokuwa bondeni baada ya kuukwea mlima Ikindika. Matumaini yakarejea japo
hawakujua maisha ya mateso yao yangekuwaje.
Walifikishwa
kwenye ua wa mfalme na mfalme wao akaanza kuchagua watumishi wake. Wakwanza
kuchaguliwa alikuwa Makoye, na wanajeshi wa jadi wakapiga makofi ya kushangilia
maana ndilo lililokuwa chaguo lao hata kabla mfalme hajachagua. Alimchagua na
mfungwa mwingine wa kike lakini hakuwa Masele maana mfalme alikuwa hataki
mabinti weusi hivyo Kidiga, binti mweupe akajizolea sifa ya kuwa mke mdogo wa
mfalme.
Wanajeshi
wa jadi pia walijichagulia wafanyakazi wa mashambani na wanawake wa kuoa.
Masele akaangukia mikononi mwa kamanda wa jeshi. Makoye alitamani kulia ila
akajikaza, alipomuangalia Masele pia alikuwa akilia maana alikuwa anampenda
sana Makoye. Watumwa waliobaki walipigwa mnada kwa waliokuwa na uwezo na mali
ikatunzwa kwa mfalme. Watumwa wapya walipata tabu sana kwa sababu kila
aliyenunua mtumwa alitaka kurudisha gharama ndani ya muda mfupi.
Lakini
haikuwa hivyo kwa Makoye, yeye alipewa uhuru wote wa kufanya kazi kwa moyo wake
ili kumuongezea mfalme utajiri. Haikupita muda Makoye alipewa kuwa msimamizi wa
watumwa wenzake pale kwenye utawala wa Mfalme wa Ikindika. Akawa akiwaongoza
kwa upendo na furaha hivyo kila mtumwa alimpenda sana Makoye. Hata watumwa
waliochukuliwa toka vijiji tofauti na Kanyaga walikuwa wakimpenda sana Makoye.
Msimu wa mavuno ulipofika mazao ya mfalme yalikuwa mengi na bora kuliko watu
wengine. Makoye akasimamia utunzwaji wa mazao stoo kwa mpangilio uliomfurahisha
sana mfalme. Mfalme akamuongezea wajibu wa kusimamia mifugo yake pia iliyokuwa
ikichungwa na kufugwa kwenye pori la jirani.
Makoye
alifanya kazi kana kwamba anafanya kazi yake. Maziwa ya ng’ombe yakawa
hayakatiki Ikulu. Watu walikunywa maziwa mpaka wakashangaa. Hata wafanyakazi wa
chini walikuwa wakibeba maziwa walipokuwa wakirudi majumbani kwao. Makoye
aligundua kuwa wachungaji wa mifugo walikuwa wavivu wa kukamua na waliyokuwa
wakikamua walikuwa wakibadilishana na chakula toka kijiji cha jirani.
Hakuwachongea kwa mfalme ila aliwataka kufanya kazi kwa juhudi zaidi na
walimtii.
Masele
binti Ntemi yeye alikuwa na hoja zake kule nyumbani kwa kamanda. Maana siku
alipopelekwa nyumbani kwa kamanda ambapo alikuwa na wake zaidi ya sita na kila
mmoja alikuwa na kanyumba kake. Hivyo Masele akaingia kwenye nyumba aliyokuwa
analala kamanda. Kilikuwa ni kijumba kidogo sana kwa nje ila kwa ndani kilikuwa
kizuri chenye michoro ya chokaa nyeupe, ya chungwa na nyeupe ukutani. Kulikuwa
na kitanda cha kamba chenye ngozi mbili laini juu yake.
Kamanda
akamwamuru Masele kwenda kuoga huku yeye akitumia dawa za kienyeji za kuondoa
mikosi na mabalaa ambayo vijiji alivyovivamia vingemuombea. Binti Ntemi alirudi
akitetema maana alijua lengo la kamanda yule. Wakati akioga alitamani atoroke
lakini wanawake na vijana walikuwa wengi hivyo jaribio lake lisingezaa matunda.
Akaingia ndani kwa hofu. Alishangaa kuona kuwa kamanda akimuonesha chakula na
kuondoka.
Kamanda
alijaribu jaribio lake la kumuingilia kimwili binti Ntemi lakini bila kuzaa
matunda. Alijaribu kwenda kujaribu kwa wake zake na alikuwa akifanikiwa
kuwagaragaza haswa ila alikuwa akimsogelea binti mfalme tu mawazo yake
yanamuhama. Siku uvumilivu ukamshinda akamuuliza Masele mbona yuko vile alivyo.
Masele akamwambia kuwa alikuwa amezindikwa na mizimu ya babu zake na mwanaume
ambaya angejilazimisha tofauti na inavyomwambia nafsi yake basi angekufa.
Mwanaume ambaye hata mizimu ilimkubali ni Makoye tu. Kamanda aliogopa sana na
kumpeleka kwa Makoye.
Mfalme
alimwandalia sherehe kubwa sana Makoye ili amuoe chaguo la moyo wake, Masele
binti Ntemi. Watu walifurahi kuona kiongozi wao muelewa na asiyewapa majukumu
yaliyowazidi akifunga pingu za maisha. Watumwa walifurahi utafikiri ilikuwa
sherehe yao ya uhuru. Makoye akajipatia jiko tena palepale Ikulu. watu
walikula, walikunywa na kucheza ngoma hasa.
Baada
ya sherehe ya harusi ya Makoye, mfalme alimfanya kuwa kiongozi kwenye serikali
ya kijiji chake. Kila mtu kijijini alimfahamu Makoye na aliona kama mfalme
amechelewesha uteuzi ule. Watu wote walisaidiana naye katika uongozi vizuri.
Ila alikuwa na ombi moja tu kwa mfalme endapo kungekuwa na mpango wa kukiteka
kijiji cha Kanyaga basi asihusishwe maana angejisikia hatia kubwa sana. Mfalme
alimuelewa na maisha yalikwenda vyema kuliko hata mfalme alivyokusudia.
Mafanikio
ya kijiji cha Ikindika yalikuwa makubwa mno kuliko ilivyokuwa hapo awali. Kila
mtu akajua mchapa kazi Makoye ndiye chanzo cha mafanikio yale yote. Baadaya
kikao cha tathmini ya mafanikio na dira ya kijiji kukaa, mfalme aliamua
kumtangaza Makoye kuwa ni Kiongozi wa pili katika utawala wake. Masele binti
Ntemi alipigwa butwaa kuona kuwa mumewe alipanda vyeo kiurahisi na bila
kipingamizi toka kwa kijiji cha ugeni.
Mfalme
akaanza kuugua maradhi yasiyojulikana kwa muda mrefu. Wataalamu wa tiba za
asili makundi kwa makundi walikuja ili kunusuru afya ya mfalme. Mfalme alikuwa
hawezi hata kuzungumza hivyo majukumu yote yakawa yanatolewa na Makoye na watu
walimwamini kweli. Baadhi ya wafungwa wa kijiji cha Kanyaga waliomba ruhusa ya
kurudi nyumbani kwani walikuwa wamechoka kukaa utumwani. Makoye akatengeneza
sharia nzuri ya kuwaachia huru watumwa wote maana kwa namna walivyoishi kwa
raha hata wangeondoka wangerudi wenyewe tu.
Wazee
wa baraza waliona ni wazo jema maana lingewaletea watu wengi zaidi pale kijijini
ambao wangeomba kufanya kazi za mashambani na kuchunga mifugo yao. Hivyo waraka
ukatolewa wa wafungwa wote kuwa huru na kufanya kazi kwa maelewano ya ujira.
Wafungwa wengi walifurahi kuwa huru na kwa sababu masika yalikuwa hayajaanza
basi walirudi vijijini kwao kwa matumaini ya kurudi tena wakati wa msimu wa
kilimo.
Watumwa
waliotokea Kanyaga waliopanga siku maalumu ya kurudi nyumbani. Wakatuma mjumbe
kwenda kumwambia Masele binti Malkia kuwa walikuwa wamepanga waende nyumbani
baada ya siku mbili na walimtegemea sana Makoye ili awaongoze njia. Lakini
Masele alipomwambia Makoye akawaomba sana waende na wangemkuta siku ambayo
wangerudi, maana utawala wote wa kijiji cha Ikindika ulikuwa chini yake na
mfalme angekufa yeye ndiye angekuwa mfalme.
Mateka
huru wa kijiji cha Kanyaga walisikitika sana kusikia taarifa za kusikitisha
kutoka kwa kiongozi wao waliomtegemea kuwa alikuwa akipambania maslahi mapana
ya Kanyaga. Basi Masele binti Ntemi akawa kiongozi wa msafara. Safari ilikuwa
ndefu na ngumu hasa pale walipokumbuka wamemuacha mchapakzi shujaa wa Kanyaga.
Lakini hata usiku uwe mrefu vipi huwa kuna pambazuka. Mateka huru wakaingia
kijijini Kanyaga ambapo palifanyika sherehe kubwa sana ya kuwapokea.
Kila
familia ilifurahi kukutana na mwanafamilia waliyempoteza kwa muda mrefu sana.
Lakini kwa bahati mbaya sana, kulikuwa na wazee wawili ambao walikuwa ni wazazi
wa Makoye. Walikuwa na huzuni kubwa sana na walishindindwa kujizuia walipokosa
kumuona mtoto wao mpendwa. Walidhani kuwa amefia huko kwenye utawala wa utumwa,
hivyo waliangua kilio kikubwa sana. Lakini Masele binti Ntemi aliwatoa hofu
wakwe zake na kuwaambia kuwa alikuwa mzima na walikuwa wameshaoana.
Masele
binti Ntemi aliwapa na habari njema kuwa mtoto wao amekuwa kiongozi wa pili
baada ya mfalme wa utawala wa Ikindika. Na anatarajia kuwa mfalme muda sio
mrefu maana mfalme alikuwa akiugua na angefariki muda wowote ule. Wazazi wake
Makoye hawakufurahishwa na uamuzi wa mtoto wao wa kuongoza katika serikali adui
na dharimu kwa kijiji chao. Hivyo walilipanga safari ya kwenda kumfuata. Kwa
sababu baba yake na Makoye alikuwa mzee sana alibaki kijijini Kanyaga. Safari
ikafungwa na msafara wa watu watatu, Mama yake Makoye, mke wake na mdogo wake
makoye.
Safari
huwa inakuwa karibu kwa anayekufahamu aendako tu, wengine wote hutunza nguvu
muda wote. Masele alikuwa anakufahamu kijijini Ikindika ila waliobaki walikuwa
wanacheza mchezo wa kubahatisha tu. Walipanda milima, wakavuka mito na mabonde
mpaka wakafika katika kijiji cha makatili wasio na haya, Ikindika. Masele
aliongoza njia mpaka Ikulu maana alikuwa akifahamika sana. Wazee walishangaa
yaani kaondoka jana tu na leo karudi, ama kwa kweli nchi ya Ikindika ilikuwa
imebarikiwa.
Makoye
aliitwa nje ya Ikulu, alishangaa kumuona mke wake aliyeondoka jana tu. Lakini
alipotoka nje na kumuona mama yake machozi yalimlengalenga kwa huruma na furaha
kwa wakati mmoja. Mama yake aliyekuwa mnene na mwenye afya njema leo alikuwa
amekonda na kuzeeka mno. Akauliza na yule mtu wa tatu alikuwa nani, akaambiwa
alikuwa ni mdogo wake aliyemuacha na miaka kumi. Alionekana kuwa kijana wa
makamu na mwenye nguvu.
Mama
hakupoteza muda akamwambia kijana wake abebe kila kilicho chake warudi
nyumbani. Lakini majibu ya Makoye yalimchosha sana mama yake, maana alimwambia
alikuwa amemuandalia na kumjengea nyumba ili waje waishi katika nchi ya
Ikindika. Mama alijaribu kumkumbusha kuwa watu hawa ndio waliowauwa ndugu zake
kipindi cha uvamizi na jeshi la Ntemi mpya, Nchemu lilikuwa linajipanga kulipa
kisasi kwa serikali hii ya ikindika. Jitihada zote ziligonga mwamba,
akawatawanya kwa kuwaambia kuwa wasubiri angewatumia mtu siku ya kutawazwa
kwake.
Mama
yake na Makoye hakuamini masikio yake. Alilia chozi la huzuni na kumuaga mtoto wake
aliyekuwa akimuwaza kwa miaka kumi na miwili. Walianza safari ya kurudi
kijijini Kanyaga wakiwa na maumivu makubwa ya moyo kwani ukitegemea kitu halafu
ukakikosa moyo huwa mzito sana. Uzito wa mioyo uliilemea miguu kutembea. Sehemu
ambayo walitumia masaa matatu kuja waliyumia masaa nane kurudi. Maana mama alikuwa
akifika kwenye jiwe anakaa na kulia sana huku akijiuliza kilimpata nini mtoto
wake mpenzi. Chelewa ufike, walifika kijijini Kanyaga mnamo saa nane usiku
wakiwa hoi wa miili na roho.
Huku
kijijini Ikindika mambo yalionekana kumnyookea Makoye, maana hata kabla mama
yake hajafika nyumbani, mfalme akaaga dunia. Moyo wa Matatizo ulikuwa na furaha
sana ijapokuwa usoni alionekana kuhuzunika sana. Kwa sababu ilikuwa usiku basi
alijitahidi kuitisha vikao vya hapa na pale ili kujua namna mambo ambavyo yangeenda.
Hata kama ukifa wenzako wanakula chakula na wanalala kama ilivyokuwa kawaida.
Makoye na viongozi wengine walitawanyika kwenda kujipumzisha kwenye nyumba zao.
Alibaki
malkia tu na majirani wachache wakilia usiku kucha. Usiku ule Makoye alitamani
apate mtu wa kushirikiana nae furaha yake ya kuwa mfalme katika nchi ya ugenini.
Alijikuta akikesha tu kitandani na kujigeuza huku na kule kama mlango wenye
bawabu mbovu. Mara ghafla kitu kama ndege kikatua juu ya paa lake kwa kishindo.
Makoye akalala chali na kuomba awe na macho yanayoona hadi nje. Japo alikuwa
sio muoga lakini hakupendwa kushituliwa hasa wakati wa usiku. Wakati mawazo
yakitafuta ni nini kilikuwa juu ya paa lake bundi alilia kwa sauti ya huzuni
tofauti na milio ile ya kawaida.
Wakati
akifikiria zaidi cha kufanya bundi alikuwa akili kwa huzuni. Wazo likamjia
kichwani kuwa watu wa Kanyaga wamemtumia bundi ili kumuogopesha arudi nyumbani.
Akaamka toka kitandani kwake akachukua upinde wake na mishale akatoka nje.
Akamvizia yule bundi wakati bundi analia milio yake ya huzuni Makoye akawa
akilenga shabaha yake. Alipomuweka bundi kwenye shabaha akaachia upinde wake.
bundi alisikia sauti ya kitu kikivuma akaandaa mabawa yake kuruka, alikuwa
amechelewa sana. Mshale wa Makoye ukampata kifuani na kumuangusha upande wa
pili wa nyumba.
Makoye
akamfuta akauinua upinde wake bundi alikuwa mwisho wa upinde akipambania pumzi
yake ya mwisho. Makoye akajisemea moyoni tutaona nani atakaye warudishia
taarifa. Akamchukua bundi vile vile kwenye upinde wake akaingia nae ndani. Akakaa
kitandani, akawasha kibatari chake akimwagalia bundi yule alipokuwa akikata
roho. Bundi alipokata roho tu, akakumbuka mazungumzo ya mama yake, ‘‘huwezi
kumgeuza adui yako akupende bila sababu ya msingi, njia nzuri ya kuishi na adui
ni kukaa nae mbali.’’ Akazima kibatari chake na kulala usingizi mzito kutokana
na kazi nzito alizozifanya mchana kutwa.
Asubuhi
ilikucha kama asubuhi nyingine, Makoye aliamka ili aanze shughuli za siku iliyo
mbele yake. Akaamka kitandani ili anawe uso maana jua lilikuwa linamchungulia
kupitia uwazi wa madirisha yake. Makoye alipoangalia chini akaona mshale wake
tu ndo umechoma chini. Ndege wa mabalaa bundi hakuwepo, akaangalia uvunguni mwa
kitanda palikuwa patupu. Kuzunguka chumba chake hapakuonesha hata unyoya wa
bundi. Akajisemea moyoni mwake kama angeendelea kusumbuka na kumtafuta bundi
yule angechelewesha ratiba za mazishi ya mfalme. Hivyo akajipaka maji usoni na
kuondoka.
Alipofika
nyumbani kwa mfalme akakuta watu wengi wakitikisa vichwa vyao na kumnyooshea
vidole. Moyoni akajua kuwa uchifu ameshaupata. Alitaka kuingia ndani lakini
walinzi walimzuia wakamwambia kuna kikao cha wazee kilikuwa kikiendelea ndani.
Baada ya muda mfupi kiongozi wa wazee alitangaza watu kuelekea sehemu ambapo
lilikuwa limechinjwa kaburi la mfalme. Na baada ya mazishi tu angetangazwa
mfalme mpya wa Ikindika.
Watu
wote walisogea kwenye kaburi, kiongozi wa mila akaingia kaburini na kunyunyizia
damu ya ng’ombe kwenye kuta za kaburi na baadae kutoka. Tanganzo la kuushusha
mwili wa mfalme kaburini lilitolewa na mwili ukashushwa kaburini. Kabla ya
kumfukia, mzee wa mila alitangaza kuwa mfalme huwa anazikwa na mtu wa karibu
sana. Mtu aliyekuwa anafanya maamuzi ya serikali hii kwa niaba ya mfalme. Na
kuongeza kuwa wazee wote walipendekeza kuwa Makoye ndiye atakayezikwa na
mfalme. Makoye alikamatwa kabla hajaongea neno akatumbukizwa kaburini. Vijana
wakaanza kumfukia mpaka udongo ulipoisha. Makoye akazikwa akiwa mzima na cheo
chake cha usaidizi wa mfalme mkononi.
HADITHI YA 6: LEMI, AJUZA MCHAWI.
Wakati
wa utawala wa Ntemi Nchemu Amani na heshima ya kijiji cha Kanyaga ilirudi.
Alikuwa amechagua jeshi lake aliloliita Sungusungu. Sungusungu hawakuwa kwa
jina bali walikuwa kwa vitendo. Kama ambavyo wadudu sungusungu walivyokuwa
wanaweza kushambulia ganda la muwa kwa uhakika na kwa dakika chache tu ganda la
muwa lilikuwa likiachwa likiwa kavu kabisa.
Wanakijiji
wa Kanyaga walikuwa wakiheshimu msafara wa wadudu walioitwa sungusungu. Kwa
sababu wadudu hawa walipotibuliwa msafara wao walikuwa wakimpanda mtu kimya kimya
na kuanza kumuuma wakiwa ndani ya nguo tiyari. Hivyo mtu hujikuta akipiga kwata
ya bila kuamrishwa na kutamani kuvua nguo zote hata mbele za watu.
Kuna
hadithi inapigwa na wazee wa Kanyaga kuwa kuna kijana alienda kutoa mahari
ukweni. Sasa kwa heshima na kuwaogopa wakweze akaomba akae sehemu ambayo
ilikuwa na ukoka ili awe mbali japo kidogo na wakwe zake. Kwenye ukoka
palimwangwa makombo ya wali. Kwa sababu makombo yalikuwa tu, kidogo kijana hata
hakuyaona akaketi. Sungu sungu wakampanda kupitia mikononi na miguuni kasha
wakaanza kumngata haswa haswa bwana harusi tarajali. Uzalendo ulipomshida
alitoa shati na kuanza kukimbia kama mwehu.
Hilo
ndilo jeshi la Sungungungu lilivyokuwa likiogopwa na vijiji vyote
vilivyokizunguka kijiji cha Kanyaga. Walikuwa wanashambulia bila kuchoka na kwa
kupokezana. Wanakijiji wa Kanyaga walijisikia kuwa na uhuru hata wa kuacha mali
zao nje kwa sababu sungusungu walikuwa wakizunguka hata usiku wa manane kukagua
usalama wa kijiji.
Watu
wapenda Amani wa vijiji vya mbali walikuwa wakija kujitafutia hifadhi kijijini
hapo. Wazee kwa vijana walikuwa wakionekana kuja na kulowea kijijini Kanyaga.
Masharti ya kuhamia hata hayakuwa magumu. Muombaji alipaswa kwenda kwa jeshi la
sungusungu na kukaguliwa mali zake zote. Kisha alitakiwa kutumika kwa
mwanakijiji mwenyeji kwa mwaka mzima ili ampe eneo lake la kujenga nyumba na
kuendesha shughuli zake hapo.
Moja
kati ya wahamiaji wa kijijini pale alikuwa Lemi, ajuza. Kwa sababu ya uzee wake
sungusungu hata hawakuwa na adhima ya kukagua vifurushi vyake kwani walimuona
kutokuwa na madhara yoyote kwa kijiji chao. Watu wa Kanyaga walikuwa na huruma
pia basi walimtafutia eneo ajuza Lemi bila ya kumtumikisha kwa kazi za
mashambani kwa mwaka mzima.
Ajuza
Lemi akawa sehemu ya familia kubwa ya kijiji cha Kanyaga. Mwanzo watu
walimshangaa kuona ajuza akijenga nyumba kubwa na nzuri kuliko hata za wananchi
waliowengi pale kijijini. Wakadhani kuwa alikuwa na elimu ya uwashi au pengine
mumewe, ambaye alisema alikufa miaka mitano iliyopita, alikuwa fundi mwashi.
Siku
hazigandi wala kurudi nyuma, huwa zinasonga mbele tu. Ajuza Lemi akawa anakodi
mashamba makubwa na kupata mavuno mengi sana. Kuna mwaka alipata magunia mia
tatu ya mahindi na magunia mia tatu na kumi na tano ya mpunga. Lakini
kilichowashangaza watu wengi, alikuwa hauzi na mwaka mwingine anaingia shambani
kulima tena kwa wingi zaidi.
Wanakijiji
walipopata shida za chakula ajuza hakusita kuwasaidia tena bila kuhitaji
kurudishiwa. Wanakijiji wakampenda sana ajuza akawa ndo kimbilio la wavivu wa
kazi pale kijijini. Ajuza akawa akiheshimiwa sana pale kijijini kwa sababu ya
roho yake ya ukarimu.
Kuna
siku ajuza alikuwa akiulizia mbuzi wa kununua maana anasema alipata ujumbe wa
ghafla ndugu zake wangekuja kumtembelea jioni ile. Basi wale waliokuwa wanakula
vya bure wakamwambia ajuza apumzike na kwamba wangemsaidia kumletea beberu
aliyenona kwa gharama nzuri tu. Kweli juhudi huwa haidanganyi, beberu la miaka
mitatu lililokuwa likinuka vumba lilipatikana kwa gharama ya gunia moja tu la
mpunga.
Ajuza
alifurahi kuona beberu kubwa namna ile kwa gharama iliyokuwa sawa na bure. Wala
vya bure wakapima mpunga na kwenda kumkabidhi aliyetoa beberu na kumuhakikishia
kuwa wangekuwa pale alfajiri kwa ajili ya kumsaidia kuchinja na kumchuna beberu
yule.
Asubuhi
waliamka wako hoi sana vijana wale. Walijitahidi kujikongoja ili wawahi
kumsaidia ajuza kazi ya uchinjaji na uchunaji wa beberu lake la sherehe.
Walishangaa kutokutana na mtu hata mmoja njiani. Watu wa Kanyaga walikuwa
wanaamka mapema kila siku hata kipindi cha kiangazi kwa sababu ya shughuli za
kulima bustani zao zilizopo mabondeni. Ila leo hawakukutana hata na mwanajeshi
mmoja wa sungusungu. Walipiga moyo konde na kuendelea na safari yao.
Walifika
nyumbani kwa ajuza ili kumsaidia shughuli waliyokuwa wamemuahidi jioni
iliyopita. Walikuwa wamechelewa kidogo tu maana walikuta ajuza anaingiza chungu
cha damu ndani. Walipomuangalia beberu alikuwa ameshajichwa na kutundikwa
kwenye mti wa mzambarau uliokuwa karibu na nyumba ya ajuza.
Baada
ya ajuza kutoka nje tena, vijana wakamuuliza kama angemchuna ngozi yeye
mwenyewe. Ajuza aliwaambia hakuhusika na kumchinja yule beberu bali kuna kijana
alipita na kumpa msaada tu. Walafi huwa hawachunguzi sana chakula, waliomba
visu na kuanza kumchuna yule beberu. Vijana waliona kama alama ya meno ya
mnyama mkali kwenye paja la kushoto la beberu yule. Wakati wakishangaa ajuza
aliwaambia kuna mbwa alitaka kumla beberu yule baada ya kuchinjwa kwani alikuwa
ndani.
Vijana
walipewa mabakuli makubwa ya supu ya utumbo na nyama za ndani wakati wakisubiri
chakula kiive. Walikunywa supu na kumshukuru ajuza. Walitamani kuaga kuondoka
ili warudi nyumbani na baadae wangerudi kwa ajili ya kuonja pishi la wageni
lakini haikuwezekana. Usingizi mzito uliwapitia kwenye viti walivyokuwa wamelalia.
Ajuza aliingia ndani na kutoka na mkia wa fisi akawagusa wale vijana wawili kwa
mkia wake wakageuka kuwa fisi palepale. Akawaswaga wakaingia ndani.
Wazazi
wa wale vijana walidhani vijana wao wameenda kumwagilia bustani hivyo
hawakuwatafuta. Lakini ilipofika jioni walishangaa kuona vijana hawarudi
nyumbani. Walipowauliza rafiki zao, walijibu hawakuwa wamewaona mahali.
Walienda kwa ajuza kuwaangalia, maana walijua watakuwa wanakula sherehe kama
walivyosimulia jioni yake. Cha ajabu walipofika kwa ajuza hapakuwa hata na
dalili ya sherehe au hata harufu ya nyama.
Walishangaa
kumuona ajuza akisonga ugali wake na Nsasa,
mboga za majani zilizokaushwa. Walipomuuliza kama aliwaona vijana, ajuza
akaruka maili mia nane. Alisema yeye mwenyewe alikuwa amempoteza beberu wake.
Hivi ndio alikuwa anaingia toka kumtafuta beberu wake na hakumpata. Wazazi wa
wale vijana walimpa pole ajuza na kuzidi kuwatafuata vijana wao bila mafanikio.
Watu
walidhani kuwa hawa vijana wameraruliwa na wanyama wakali au wamemeza na chatu.
Lakini walienda saa ngapi na kufanya nini huko porini, maswali yalikosa majibu.
Wazazi wa wale vijana wakaita msiba na watu wakahudhuria kulia msiba usio na
mazishi. Kulia bila kuiona maiti nayo inashida zake maana waliaji wengi
walishindwa kulia kihaswa haswa kama kwenye misiba mingine. Hivyo ndivyo vijana
walivyosahaulika pale kijijini.
Msimu
wa kilimo uliofuatia ulianza na watu walianza kazi zao za mashambani kama
ilivyokuwa kawaida yao. Ajuza akaongeza kukodi mashamba mara dufu. Wanakijiji
walijishangaa kila wakiamka asubuhi walikuwa wachovu mno na hata wakati
mwingine kuahirisha shughuli za shamba kwa siku husika. Lakini hata wangeamka
kesho yake walijikuta wachovu zaidi ya ilivyokuwa jana.
Baadhi
ya wanakijiji walijua labda uzee ulikuwa ukiwanyemelea. Lakini cha ajabu hata
vijana walikuwa wakilalamika kuchoka sana tena isivyokawaida. Wanakijiji
wakaanza kufa mmoja baada ya mwingine. Wakawa wakishauriana kupunguza ukubwa wa
mashamba maana afya zao zilikuwa za muhimu kwa maendeleo ya kijiji. Lakini wapi
bwana, uchovu ukawa kama sehemu yao ya maisha.
Ntemi
alipata malalamiko na kuitisha mkutano wa kijiji na kuwaomba wanakijiji wake
wapumzike kufanya kazi kwa wiki nzima labda mambo yangetulia. Wiki iliisha na
watu walikuwa wachovu kila uchwao. Usiku mmoja Ntemi aliamka usiku wa manene na
kutoka nje ya Ikulu, maana alisikia sauti ya mtu akitwanga kwa kutumia kinu.
Alipotoka nje hakuona mtu anayetwanga bali alisikia sauti za vinu zaidi ya
kimoja vikitwanga tena bila kupumzika.
Ntemi
aliogopa kwenda kuchunguza na kupanga kwenda kumtafuta mganga kijiji cha pili
maana aliona kama mauza uza na hakujua haswa ni nani aliyehusika na tukio hilo.
Ntemi usingizi ulimpaa maana hata hao sungusungu wake anaowategemea hakuwaona
kwenye doria ya usiku. Mawazo mengi sana yalimjia kichwani ikiwa ni pamoja na
kumshuku mganga wa kijiji maana alikuwa amemkatalia ombi lake la kuutumia msitu
wa tambiko kwa tambiko lake binafsi.
Asubuhi
iliyofuata ilikuwa ya vituko zaidi maana wanakijiji wanne ambao hawakwenda
shamba siku iliyopita walijikuta wanaamka na tope jeusi la majarubani.
Wanakijiji wakaanza kulalamika kuchezewa. Kiongozi wa sungusungu pia akatoboa
siri kuwa jeshi lake lilikuwa halifanyi doria za usiku kwa sababu wanakuwa
wamechoka na wakisema wajipumzishe tu, huwa wanaamka kumekucha.
Ntemi
aliamuru baragumu lipulizwe na watu wasogee eneo la mikutano ya kijiji. Ntemi
alikuwa amefura sana hata kuongea kwake ni kama alijilazimisha tu. Aliwasimulia
kuhusia na vinu vilivyokuwa vinatwanga usiku kucha. Hakuna aliyekuwa na taarifa
au kukiri kuwa alikuwa akitwanga usiku. Aliamua kukitambulisha kikundi cha
waganga maarufu kwa kuwakamata wachawi toka kijiji jirani.
Wanakijiji
wa Kanyaga wakawa wanashangaa tu maana wamechoka na hawajui sababu za kuchoka
kwao. Ngoma za kumsaka mchawi zikaanza kulia. Waganga wakacheza haswa mpaka
nyasi walizokuwa wakizikanyaga zikakauka. Baada ya muda kiongozi wa ngoma
akanyoosha mkono na ngoma pamoja na wachezaji vikasimama. Mganga akasema mizimu
yake imemwambia kuna mtu anawachezea raia wa Kanyaga.
Kuna
mtu mmoja anawalimisha raia wote kwenye mashamba yake ya mahindi na mpunga. Na
pia huwa anawatwangisha na kuwasagisha watu usiku kucha ili awalishe misukule
wake. Kwamba siku za mtu huyo zilikuwa zimefika kikomo. Akawaambia wakati ngoma
zinapigwa kwa mara ya mwisho ajitokeze mara moja ili wawe na mazungumzo nae
huenda wangemsamehe.
Ngoma
zililia, waganga wakacheza mpaka jasho lakini hakuna aliyesimama kujisema kuwa
ndiye mchawi. Mganga akavaa kofia yake yenye manyoya ya bundi na miiba ya
nungunungu. Akaanza kuongea kuwa yeye alikuwa hamfahamu raia hata mmoja
isipokuwa Ntemi tu lakini mizimu yake ilikuwa ikimfahamu kila mtu pale.
Akjiwekea ugoro puani na kupiga mfululilizo wa chafya akaanza kukimbia kama
mbwa mwenyekichaa kumtafuta mchawi.
Baada
ya kuzunguka wanakijiji wote alijirusha kati kati ya wanakijiji na kumkamata
ajuza. Ajuza hata hakuonesha dalili za kuogopa mwanzoni. Akampeleka mbele ya
wanakijiji wote. Ajuza alikuwa amevaa kaniki yake, mganga akaivua na kupandisha
blauzi yake juu. Looh! Ajuza alikuwa na rundo la hirizi na shanga kuzunguka
kiuno chake. Mganga alizivuta shanga na hirizi kwa mkono wake wa kushoto na
kuzikata. Kasha akaamuru wasaidizi wake wazichome moto pale pale.
Baada
ya hapo wakati watu wanazidi kushangaa, mganga alimwamuru ajuza kuachama. Mganga
aliongea maneno yasiyoeleweka halafu akaingiza vidole vyake chini ya ulimi wa
ajuza. Mganga akaonekana kama akihangaika kushika kitu kilichokuwa kikitereza
toka ulimini mwa ajuza. Mara akavuta kwa nguvu, watu wakaruka na kupiga mayowe.
Maana alitokea koboko mmoja mrefu kimo cha mgaga ila mganga alikuwa amemshika
kichwa chake kwa nguvu na kumuua.
Mganga
aliomba kipande cha chupa na kukitumia kumnyoa ajuza nywele zake. Alipomaliza
kumyoa akaomba dawa ya unga iliyokuwa kwenye kikopo kidogo na kuupaka upaa wa
ajuza. Akatangaza kuwa ajuza yule endapo angeurudia uchawi au kuficha kitu cha
uchawi angekufa palepale mkutanoni. Akamwamuru ajuza aseme mbele za wanakijiji
ni wapi alikuwa ameficha uchawi wake mwingine.
Ajuza
hakuwa mbishi akasema upo nyumbani kwake. Mganga akasema ajuza yuko sahihi
twendeni mkaone mambo ya ajuza. Watu walishikwa na butwaa kuona ajuza
waliyemwamini na kumuona kimbilio wakati wa shida zao kumbe alikuwa mchawi wa
kupindukia. Waliowahi kula chakula kwa ajuza walikuwa wakijaribu kujitapisha
bila mafanikio.
Walipofika
nyumbani kwa ajuza watu wengi walijaa mlangoni pa nyumba ya ajuza wakisubiri
kuingia kujionea uchawi wa ajuza. Lakini mganga alipokuja aliwaomba wakae mbali
ka mita mia maana kulikuwa na hatari mule ndani. Wanakijiji kusikia hatari
walikaa umbali wa mita mia tatu hivi. Ajiza akafungwa kamba kwenye mzambarau
wake hata hakuweza kujitikisa. Mganga alivaa kofia yake na kuanza kuizunguka
nyumba huku akiinyunyizia dawa.
Baada
ya zoezi la kuizunguka nyumba mganga alienda mlangoni na kumwaga dawa nyingi
pale mlangoni. Mganga aliupiga teke mlango na kusema ‘‘Fumagako.’’ Walianza
kutoka fisi waliokuwa wanakimbia kawa wamewashwa moto mgongoni. Wanakijiji
walikuwa wakihesababu tu mpaka wakafika fisi mia tano na themanini. Mara ghafla
bundi nao wakaanza kutoka kwa vurugu zote. Wanakijiji walishindwa kuwahesabu
bundi kwa sababu walikuwa wanaruka bila mpangilio.
Mara
chatu akaonekana akijisukuma kutoka nje, watu wakataka kumenya mbio lakini
alipofika jirani na mlango na kuigusa ile dawa ya mganga aliyeyuka. Palipokuwa
kimya mganga akamuita Ntemi wakaingia nae ndani na mganga akamuonesha kitu
Ntemi lakini Ntemi hakuwa anaona kitu. Mganga akachukua dawa akampaka machoni,
mara Ntemi akaduwaa.
Walipotoka
nje tu, watu walikuwa wamejaa mlangoni. Ntemi uzalendo ukamshinda akasema
jamani wale watu waliopotea na waliokufa tukawazika wamo humu ndani. Watu
wakajawa na shauku ya kuwaona. Mganga alikuwa mstaarabu akawaambia kwa sasa sio
watu tena bali ni misukule. Hawawezi kuishi kama binadamu tena kwa sababu
wamekatwa ndimi na wanatisha sana. Nitafanya dawa ili waende kwenye makaburi
yao. Wananchi wa Kanyaga hawakuwa wakatiri ila ajuza huyu aliwaamshia hasira
kali sana. Mganga alikuwa mtu mstaarabu sana akawaambia kwa sababu wamesha
muadhibu ajuza yule ilikuwa haina haja ya kumdhuru. Wanakijij walimbeba ajuza
mzega mzega na kwenda kumtupa nje ya mipaka ya kijiji cha Kanyaga. Wakampa onyo
kuwa sasa hivi wamemuacha hai ila akirudi tena kijijini watakuja kuitupa mifupa
yake pale mpakani ili iwe fudisho kwa wachawi wengine.
HADITHI YA 7: NJAA KALI YAIKUMBA
KANYAGA
Baada
ya kumfukuza ajuza mchawi toka kwenye mipaka ya kijiji cha Kanyaga, wanakijiji
walianza kulala kwa raha mustarehe. Baadhi ya wanakijiji waliamua wafidie
usingizi kwa siku ambazo walikuwa wakitumikishwa kwenye mashamba ya ajuza
mchawi. Akili ya mwanadamu imeumbiwa kusahau, ajuza akasahulika kabisa pale
Kanyaga. Maisha yakarudi kama ilivyokuwa awali, watu wakawa wakiamka alfajiri
kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli za mashamba yao.
Lakini
kwa bahati mbaya sana msimu huu haukuwa na mvua za kutosha. Mwanzoni mwa msimu
mvua zilianza kunyesha vizuri na wakulima wa Kanyaga wakalima na kupanda mazao
yao. Wakawa wakiyapalilia ili kuondoa magugu yaliyokuwa yakiisumbua mimea
isikue kwa usahihi. Kila mkulima alikuwa amemaliza palizi ya kwanza na wakawa
wanasubiri palizi ya pili ambayo ndio ilikuwa palizi ya mwisho na ya muhimu
sana.
Palizi
ya pili ilikuwa ni ya muhimu kwa sababu ilisaidia mimea kubeba watoto wenye
afya zaidi. Wakulima walikuwa wakiisubiria palizi ile ije bila mafanikio. Maana
jua lilikuwa kali kiasi cha kuanza kukausha mazao na magugu madogo madogo
yaliyokuwa yameanza kuota. Wakulima wa Kanyaga wakaanza kutia hofu kama msimu
ule ungeleta mazao ya kutosha maghalani mwao.
Mara
moto wa ajabu ukavamia mashamba yao. Ukaunguza kweli mahindi na karanga
zilizokuwa mashambani. Moto ukaingia msitu wa jirani na kijiji na ukawa ukiimba
usiku na mchana na miti ya mwituni. Siku ya tatu moto ukavuka msitu na kufika
sehemu kulipokuwa na majaruba ya mpunga. Huko nako kukawa na kilio kwa wakulima
wa Kanyaga. Moto ulipo kula sehemu kubwa ya mpunga ndipo uliamua kuzimika
wenyewe.
Ntemi
Nchemu akaamua kuitisha bunge la
wazee na kujadili muongozo wa kusaidia jamii nzima ya Kanyaga. Wazee wenye mvi
zao wakamshauri Ntemi, kuwambia wakulima watafute mbegu za mihogo na marando ya
kutosha ili waweze kupata japo chakula cha kuwafikisha msimu ujao wa kilimo.
Ntemi
aliwakusanya wanakijiji wake kwa baragumu na kuwaasa watafute mbegu za mihogo
na marando na wazipande. Halafu Ntemi na viongozi wake wangeenda kutambika kwa
ajili ya kupata mvua. Wanakijiji wakaanza msako wa mbegu za mihogo kuanzia ile
michungu hata ile iliyo mitamu kwa hofu ya njaa. Hakuna mwanakijiji aliyekuwa
na ujasiri wa kutaka kuishuhudia njaa. Marando yalileta ugumu kupatikana pale
kijijini kwa sababu wengi walikuwa hawapendelei kula viazi vitamu. Hivyo basi
kila mtu kwa wakati wake alikuwa akitembelea kijiji cha jirani na tela lake kwa
ajili ya kuomba marando ya viazi.
Wakalima
matuta kama walivyoelekezwa na kupanda mbegu za mihogo na marando ya viazi.
Kila mkulima alipomaliza kulima na kupanda kwa kadiri alivyoweza basi Ntemi
akaongoza wazee kwa ajili ya tambiko la mvua. Mvua kubwa ilinyesha siku ile na
watu wakafurahi kujua kuwa angalau wangeambulia mihogo na viazi. Mvua
ziliendelea kuwa za mfululizo na kusaidia mazao kwenda vizuri bila ya bugdha.
Mpunga
pia ambao haukuungua ulirudi katika hali yake na ukabeba masuke yake. Lakini
mpunga haukuwa mwingi sana wa kukidhi mahitaji ya kijiji kizima. Watu wengi
walipungukiwa chakula cha akiba kwa kasi na wakawa wakiombea viazi vikomae
waanze kuvila. Viazi huwa havichelewi baada ya majuma kumi na sita tu kila
mwana Kanyaga akawa akishikilia kiazi cha kuchoma, cha kubanika au cha
kuchemsha.
Wana
Kanyaga walikula viazi haswa mpaka vikaanza kuwakinai. Na ubaya wa viazi vitamu
bwana huwa havitunziki shambani. Baada ya miezi miwili toka vikomae vikaanza
kushambuliwa na wadudu waliokuwa wakivibugua. Panya bubu nao hawakuwa nyuma
wakaanza kupita chini kwa chini, tuta hadi tuta wakibuguna viazi vitamu. Ishara
ya panya buku ni rahisi tu ukikuta udongo tifutifu shambani kwako matuta matuta
ujue yuko kazini.
Walinyeshewa
na mvua nyingi ikabidi kutoa elimu. Wazee hao walidai njaa kama hiyo iliwahi
tokea kijiji cha mbali cha Ntemi Mahinyila. Wanakijiji wa ntemi Mahinyila
walilima viazi na vikaanza kuharibiwa na wadudu waharibifu. Mizimu ikamfundisha
namna ya kutunza chakula kwa njia salama. Aliwaamuru wanakijij wake wavune
viazi vyote na wakavimenya. Akawaamuru wachukue mapipa na kuvichemsha. Kisha
wakavianika juani. Jina lililopendezwa na mizimu ni Matobolwa, mpaka leo hii wanakijiji wale wanatengeneza matobolwa
kama kumbukumbu yao.
Hiyo
ilikuwa kijiji cha Mahinyila, na hapa tuko Kanyaga. Wazee walishauri viazi vyote
vimenywe na kukatwakatwa vipande vidogo vidogo. Kwa sababu viazi vingetenezwa
kwa aina moja vingewakinai watumiaji, mizimu ilipendekezwa vingine vianikwe
kwenye mawe mpaka vitakapo kauka na vitaitwa Michembe.
Wana
Kanyaga walitengeneza Michembe na Matobolwa kwa kadiri walivyoweza. Na
kila mtu alitunza katika ghala yake. Wanakijiji walikuwa wakinywa uji au ugali
wa Michembe kwa maziwa mgando kila uchwao. Wengi walikikinai kile chakula
lakini walikuwa hawana chaguo linguine. Hivyo wengi waliamua kunywa mtindi tupu
au hata kushinda njaa ili wapate hamu ya kula michembe au Matobolwa usiku.
Njaa
ilizidi kuwa kali, wanakijiji wakajikuta wakiachana na desturi ya ukarimu kwa
sababu maghala yalikuwa hayana vyakula. Ulikuwa ukimtembelea rafiki yako au
ndugu yako hata kama alikuwa na ratiba ya kupika na kula alikuwa akikusubiria
uondoke ndipo apike na kula na ndugu wa nyumbani kwake tu. Njaa ikaleta
utamaduni mwingine na watu wakaupokea. Hakuna aliyediriki hata kubeba ujauzito
kwa sababu ya njaa.
Njaa
inaweza kuugeuza mzimu mwema kuwa shetani, wanaume waliambizana walipokuwa
wakicheza bao. Kuna mwanaume alienda kumtembelea rafiki yake na akakuta chungu
kipo kwenye mafiga na kwa makadirio usingepita muda mrefu bila ya chakula
kupakuliwa. Lakini cha ajabu, mama wa familia akakaa mbali akisubiri mgeni
aondoke. Alipoona mgeni haondoki akachuku maji akaweka kwenye kalai, akayapooza
na kuanza kwaogesha watoto mchana wa jua kali.
Njaa
uwe unaisikia tu kwenye hadithi. Njaa ni mwanaharamu anayekera na hauwezi
kumuondoa akikuvamia. Hata watoto waliokuwa wakijifunza kutembea walijua kuwa
njaa ilikuwa imewatembelea. Maana hakuna mtoto aliyekuwa akibembelezwa kula.
Sufuria la uji wa Miichembe lilikuwa likigombaniwa na wakubwa kwa watoto.
Maghala
mengi yakaishiwa chakula. Watu wakaanza kuwa wehu wakijiongelea tu wenyewe
njiani. Ngombe na watu walikonda mpaka mbavu zikafanan na nyuzi za zeze.
Familia zenye mifugo wakaanza kuchinja ng’ombe na kumkausha ili awe anawasukuma
kwa muda mrefu. Wasio na mifugo wakawa wakikopa mbuzi kwa wenye mifugo kwa
ahadi ya kurudisha magunia matano ya mahindi baadae.
Njaa
rafiki yake mkubwa ukame. Basi ukame akaja kumsaidia rafiki yake kazi ya
kuwanyoosha wana Kanyaga. Wanakanyaga walinyooshwa na wakanyosheka haswa.
Wazazi wakaanza kuchukia salamu za asubuhi kwa kuona ni kelele tu masikioni
mwao. Mabwawa ya maji ya kijiji yalikauka yote. Wanawake wakawa wakifuata maji
maili nyingi na kurudi kwa kuchelewa.
Maji
yaliadimika hata vijiji vya jirani kwa hivyo yakaanza kufuatwa mbali tena kwa
matela ya ng’ombe. Mabinti wengi waliolewa kwa ajili ya umbali wa kufuata maji.
Wengine sahani ya ugali kwa uadimu wake iliwafanya wahamie kwa wavulana wa
kijij kile. Miwa pia iliwasababisha mabinti wengi waolewe kwa muda au jumla.
Hakuna
mtu aliyeheshimika kama mwanamke wa Kanyaga. Licha ya shida zote hizo lakini
hakuwepo hata mmoja aliyediriki kusaliti ndoa yake kwa sababu iwayo yoyote ile.
Walikubali kurudi hata usiku wa manane ilimradi waje waihudumie familia yao
hata kama ni kwa kuchelewa. Wanaume wa Kanyaga walikuwa wakicheza bao, kupiga
soga na kunywa pombe ya mkopo tu.
Ntemi
aliita wazee wa bunge lake na kwenda nao kwa ajili ya tambiko la mvua ili watu
angalau wapate maji. Tambiko lilikuwa la mafanikio lakini maji bila chakula
maisha bado yalikuwa magumu. Kwa bahati nzuri wachungaji walirudi na uyoga
uliokuwa umeota katika pori la kijiji. Basi kila mtu akakimbilia kutafuta uyoga
porini. Wana Kanyaga wakarudi na mafurushi ya uyoga na kuuchemsha ili uwe
kitoweo cha siku ile. Uliobaki ukaanikwa juani ili usioze.
Mabalaa
huwa hayabishi hodi baadhi ya wana Kanyaga walichuma hadi bhobha, ule uyoga wa njano. Uyoga huu huwa na vituko sana, maana
kuna wakati watu hula lakini hauwaletei shida yoyote. Lakini kunawakati
huwaendesha watu, kuleta kizunguzungu na kutapika pia. Wengi wa wataalamu wa
uyoga waliuepuka hata kwa matumizi. Lakini sasa ilikuwa njaa na hauna uchaguzi
mwingine. Ni kula bhobha au kushinda na njaa. Wengi waliona ni bora kula na
kujisikia kizunguzungu kuliko kushinda na njaa.
Kila
mwanafamilia jioni ile alikuwa ameshikilia bakuli la uyoga akila la kufurahia
radha tofauti ya chakula. Mara baada ya dakika kadhaa hivi wale waliokula
bhobha wakaanza kujisikia kizunguzungu. Wengine wakawa wakitapika tu. Baada ya
muda povu jeupe likaanza kuwatoka mdomoni na puani. Kesho yake asubuhi
waliokula ule uyoga wengi walikufa isipokuwa mtoto mdogo wa Ntemi Dongwe tu.
Yeye hata hakulalamika maumivu ya tumbo.
Kulikuwa
na msiba mkubwa sana pale Kanyaga. Wanasema msiba wa wengi ni sherehe lakini
hapa Kanyaga watu walikuwa wakilia sana kwa sababu hata chakula cha kupika
msibani hakikuwepo. Hata baada ya msiba walikuwa hawajui wangekula nini. Watu
waliwaombolezea ndugu jamaa na marafiki zao huku wakikosa hata nguvu ya
kuendelea kulia kwa sababu ya njaa. Walizika kwenye makaburi yaliyokuwa karibu
karibu ili kuepuka kuwachosha watu.
Msiba
haukuombolezwa siku nyingi maana watu walikuwa wakichakalika kutafuta chakula
kwa ajili walio hai. Wakagundua kuwa mihogo ya kisamvu licha ya sumu yake
lakini inaweza lika kama ingelowekwa kwenye maji kwa siku kadhaa. Maana mihogo
inayoliwa ilikuwa hata haina dalili ya kukomaa. Basi watu wakahamia kwenye
mihogo ya kisavu mpaka visamvu vyote vika kauka. Njaa ilizidisha mara dufu
makali yake.
Watu
walibadilika sura kwa kukonda wakaanza kufanana na vikaragosi. Wanaume wengi
walizitoroka familia zao na kukimbilia kusikojulikana maana waliona ni bora
wasikie familia zao zimekufa kuliko kushuhudia wakimpoteza mwana familia mmoja
baada ya mwingine. Wakina mama walisima imara kuzitetea roho za watoto wao
zivuke salama msimu ule wa njaa kali.
Ntemi
alikuwa hajawahi kusikia kuwa mizimu ingeweza kuleta chakula na watu wakala,
hivyo hata alipoombwa kwenda kuiomba mizimu hakujua akaombe nini. Alitulia
ikulu kwake akiwa na huzuni na machungu makubwa mno maana hata baadhi ya wazee
wake wa baraza walikuwa wamezitoroka familia zao. Ntemi kwa moyo wa unyonge
alimuomba kijana wake Dongwe aongozane nae ili wakatoe tambiko. Dongwe kijana
mdadisi alifurahi kwenda kudadisi msitu wa matambiko.
Dongwe
alikuwa ameshika kamba ya mbuzi alikuwa amekonda lakini akifananishwa na mbuzi
wenzake ndiye aliyekuwa mbuzi mnene kuliko wote. Dongwe na baba yake wakaelekea
msitu wa tambiko, haukuwa unatisha kwa sababu ya ukame uliopukutisha majani
yote. Hivyo Dongwe akakaa mbali akimuangalia baba yake akifanya tambiko.
Alipomaliza tu kufanya tambiko akaangalia juu na kuiamuru mvua ya Amani inyeshe
kama tambiko limekubaliwa.
Mvua
kubwa ilishuka, Dongwe na baba yake wakashika njia kuelekea nyumbani.
Walipofika nyumbani tu. Makundi ya senene na kumbikumbi yalitua katika mipaka
yote ya Kanyaga. Wana Kanyaga hawakujali mvua tena wakatoka na makapu, ndoo,
magunia na chochote ambacho kingeweza kutunza kumbikumbi na senene wale. Watu
walikuwa wanazoa na kwenda kumwaga ndani shehena na kumbikumbi na senene.
Wanakijiji walibeba senene mpaka wakachoka lakini kumbikumbi na senene walikuwa
hawapungui. Na hivi ndivyo kanyaga ilivyopona toka kwenye baa la njaa.
HADITHI
YA 8: BODO NA LAANA YA MIZIMU
Mila na desturi za Kanyaga ni kitu pekee ambacho
wanakijiji wote waliviheshimu na kuvifuata bila ya kuhoji wala kutilia shaka.
Wanakijiji wote wadogo kwa wakubwa walikuwa wakifuata mila na desturi kwa
unyenyekevu wa hali ya juu. Unyenyekevu huu ulikuwa ukirithishwa toka kizazi
kimoja hadi kingine. Wana Kanyaga walikuwa wakiamini kuwa hata mafanikio waliyo
nayo ni kwa sababu ya kufuata mila na desturi zao kwa ufasaha.
Mila na desturi hizi zilikuwa zikifundishwa katika
kila kaya wakati wa kuota moto wa jioni. Kwa sababu vijana wa kiume walikuwa
wakilala nje kwa ajili ya kulinda mifugo basi wao walipata mafunzo Zaidi kuliko
wasichana. Mvulana alikuwa akizaliwa baba wa familia. Ilikuwa mwiko kwa
mwanamke kumwita kijana wa kiume mtoto hata kama ni wakumzaa. Kama umekosa jina
zuri basi ita Ngosha, hata kama
anajifunza kutembea. Hata hivyo kanyaga walikuwa na mfumo dume ambao ulikuwa
ukilenga kumuelimisha Zaidi mtoto wa kiume ili awe kichwa cha familia bora
baadae.
Waliokuwa wanastahili kuitwa watoto ni wasichana tu.
Watoto wa kike elimu yao ilikuwa rahisi naya kuchosha. Maana walikuwa
wakifundishwa kuandaa na kutenga chakula, kupiga magoti wakati wa kukabithi
maji ya kunywa na kusalimu. Mgeni alikuwa akifika msichana wa familia
anakimbilia jikoni kupika bila kumuuliza mgeni kama ameshiba au amekula
alikotoka.
Mila na desturi ziliwajenga vijana wa kike na Mangosha wakawa watu bora wa jamii ya
Kanyaga. Kila mmoja wao alipenda kufanya vile alivyofundisha mbele ya wazazi
ili asifiwe na kuonekana hodari wa kuzingatia mila na desturi za Kanyaga.
Wazazi wa Kanyaga walikuwa wazazi wa kila kijana na Ngosha. Walikuwa hawawezi
kuvumila kuona ati mtoto akienda kinyume na mila na desturi. Ulikuwa ni wajibu
wa kila mzazi kuhakikisha kila kijana na Ngosha anaenenda sawa sawa na mila na
desturi za Kanyaga.
Lakini kila jamii licha ya ubora na muelekeo mzuri wa
mila na desturi huwa wanajitokeza vichwa ngumu. Wale wanaojifanya wana masikio
ya kufa. Wazazi wakizungumza jambo linaingilia sikio la kulia na kutokea sikio
la kushoto. Hata uwatendee wema kiasi gani wao ukengeufu ndio uchaangamfu wao.
Kila jamii lazima awepo lau mmoja au kikundi. Na kama katika jamii yako hayupo
mkengeufu, hebu jichunguze wewe mwenyewe uone.
Katika kijiji cha Kanyaga alikuwepo kijana aliyeitwa
Bodo. Huyu aliamua kuwa mkengeufu na asiyeelewa somo wala fundisho toka kwa mtu
mzima. Alikuwa akipenda kutumia lugha ya matusi tu muda wote. Ijapokuwa alikuwa
akichunga mbuzi, na usumbufu wa mbuzi unafahamika lakini yeye alitia fora.
Bodo alianza kama utani hivi. Siku moja aliligundua
jina la utotoni la mama yake kuwa alikuwa akiitwa Ngolo. Basi Bodo akawa
akimvizia baba yake akitoka tu kwenda kucheza bao au kunywa pombe basi alikuwa
akimuita mama yake kama mdogo wake. Maskini mama Bodo alikuwa mama mpole kweli,
alikuwa akiishia tu kusema ‘’sipendi uniiite hilo jina nitakuchapa.’’ Kwa sauti
ya upole kama alikuwa akimbembeleza kulala.
Utukutu wa Bodo ukaanza kuota mizizi, akawa akiwavizia
mabinti wadodo wadogo waliokuwa wakienda kuteka maji wakati wa jioni na
kuwatishia kwa kulia kama fisi kwenye vichaka vya karibu. Basi mabinti walikuwa
wakikimbia na kuvunja mitungi ya maji. Halafu Bodo hujitokeza toka kichaka cha
jirani na kuwacheka mpaka akawa akigala gala chini.
Bodo akaendelea kupamba moto, akawa akivizia wasichana
waliokuwa wakichunga ndama porini na kuwalazimisha kufanya kile alichokitaka
huku akiwapiga pale walipokuwa wakimkatalia. Mabinti wengi walikuwa wakirudi
kabla ya wakati nyumbani wakilia na kumlaumu Bodo kwa ukatili wake. Bodo akawa
akijificha porini na kurudi nyumbani giza likiingia. Wazazi wake walipomuuliza kuhusiana
na tuhuma zilizokuwa zikimkabili, Bodo aliruka maili mia mbili.
Bodo akaanza ujanja mwingine. Alipokuwa akienda
kuchunga ng’ombe na njaa ikamlemea basi alianza kuiba mahindi, viazi vitamu,
mihogo, na karanga toka kwenye mashamba ya watu. Alikuwa akirudi toka
machungani, alikuwa hali chakula alichobakiziwa na kudai kuwa rafiki zake
walikuja na gudulia ya maziwa ya mgando hivyo alikuwa bado ameshiba. Mashitaka
yalipoletwa, Bodo kama kawaida yake akakana.
Siku moja wakati wa kiangazi alibeba kijinga cha moto
kwa uficho wakati akienda machungani. Alipofika machungani akaiba viazi vya
watu akavila na kuanza kuchezea moto. Alikuwa akiwasha moto kwenye majani
makavu na kuuzima kwa miguu yake kwani alikuwa amevaa makatambuga. Aliwasha
mara ya mwisho ili aende kuwarudisha mifugo aliokuwa anachunga maana walikuwa
wameingia kwenye shaba la mahindi la jirani. Alipouwasha moto na kujiziuka
kuangalia ng’ombe upepo ukavuma ukaukoleza moto. Alidua mara kadhaa na makata
mbuga yake moto ukamzidi uwezo.
Kwa sababu alikuwa na akili nyingi akawaswaga ng’ombe
kuelekea nyumbani kwa mwendo wa mchakamchaka. Watu walimuuliza leo kulikoni
alidai alikuwa akisumbuliwa na jino hivyo alikuwa akiwahi kuchimba mzizi wa
mpapai. Alifika nyumbani na kuwafungia mifugo zizini na kujitupa kwenye ngozi
ya ng’ombe na kujifanya mgonjwa mahututi. Baada ya muda wana Kanyaga wakaona
moshi mzito ukitokea katika msitu wa kijiji.
Walifanya maalifa ya kuuzima lakini hawakuweza. Hivyo
waliamua waende kukata miti ya mbele iliyokaribiana na msitu wa tambiko ili
kuuzuia moto usijedhuru msitu wa tambiko. Walifanikiwa kuuzuia moto kwa namna
ile. Msako wa kumtamfuta baradhuri aliyefanya ule uhalibifu ulifanywa lakini
bila mafanikio. Kila waliyemuuliza alisema hajui, hata Bodo mwenyewe alisema
hajui maana jino lilikuwa likimsumbua sana. Wazee wengi walilaani kitendo kile
maana mizinga yao ya nyuki iliungua na kuwasabababishia hasara kubwa.
Yeye Bodo akawa akiboresha tabia mbaya kila uchwao.
Safari hii alikuwa akipita karibu na bwawa la maji mida ya kupunga kwa kua,
akakutana na mabinti wakioga. Basi akatafuata kichaka na kuanza kuwachungulia.
Kila ikifika jioni basi huenda kujibanza kwenye kichaka na kuwachungulia
wasichana waliokuwa wakioga. Na mbaya Zaidi alikuwa akikutana nao mmoja mmoja
alikuwa akiwaambia hadi nguo za ndani walizokuwa wamezivaa. Wasichana wengi
walimkasirikia Bodo na hata kumripoti kwa mama yake. Lakini mama yake Bodo
alikuwa akimtishia tu kumchapa.
Kuna siku moja mzazi mmoja alimkuta Bodo akimtukana
binti ambaye alikuwa ametoka kuchota maji. Mzazi alipouliza kulikuwa na nini
mpaka malumbano yao yakageuka kuwa matusi. Kumbe Bodo alimchungulia binti yule
wakati akioga na akamwambia nguo zake za ndani binti alipojaribu kukoroma Bodo
akaanza kuporomosha matusi. Basi yule mzazi akachukua jukumu la kumuadhibu
Bodo.
Bodo baada ya bakora mbili za makalioni kumuingia
kisawa sawa, akageuka kuwa mbogo. Akaamka akaidaka fimbo na kuivunja vunja.
Mzazi akaamua aanze kumzaba vibao, Bodo akampiga mweleka mmoja mzazi puuuu chini. Bodo akamkalia kifuani
akampiga ngumi na kumwagia mchanga machoni kisha akamenya mbio msituni. Alikaa
msituni kama siku tatu, wazazi wake wakabidi wamfuate na kumuahidi kuto
muadhibu endapo angerudi nyumbani.
Wazazi wengi walilaani kile kitendo kwani kilivunja
heshima ya wazazi kwa watoto pale kijijini. Wazazi wa Bodo wakaomba msamaha
ikiwa ni pamoja na kulipa mbuzi wawili kama masumule,
fidia ya adhabu. Bodo hakupunguza mapepe yake bali alizidi na kuwa mbishi Zaidi
kwa watu wazima. Siku moja baada ya kikao cha Ntemi na wanakijiji likapangwa
tambiko la Amani ya kijiji. Bodo akawanong’oneza vijana wenzake kuwa angeenda
wachungulia wazee pale walipokuwa wakifanya tambiko ili nayeye awe anajifanyia
matambiko yake.
Vijana walijaribu kuwapasha habari wazazi kutokana na
mpango wa Bodo, kwa sababu mila na desturi zilikuwa wazi hakuna aliyetilia
maanani kuwa Bodo angeenda. Mila na desturi zilikuwa zikikataza mtu asiyehusika
na tambiko kuhudhuria au hata kuchungulia tambiko. Kimsingi hakuna aliyekuwa
akiruhusiwa kuingia katika msitu wa tambiko hata kama ni muhusika siku tofauti
na siku ya tambiko. Kwa sababu kukiuka hivyo ni kujitafutia laana ya mizimu.
Siku ya tambiko ilifika, wahusika wakaongoza njia
kuelekea msitu wa tambiko wakiwa na mahitaji yote ya tambiko. Bodo nae
akafungulia mifugo kama anaenda kuichunga vile, kumbe moyoni mwake alikuwa
akipanga mipango yake. Moyo wa mtu ni msitu mnene. Wazazi wa Bodo hawakugundua
mpango wa mtoto wao. Bodo akafika machungani, safari hii alienda karibu na
msitu wa tambiko ili kutimiza azima yake. Akawaacha mifugo wake na kuanza
kunyata kwa hatua ndogo ndogo.
Aliwaona wazee na Ntemi wakiwa na maandalizi ya
tambiko, kwa sababu msitu ulikuwa ni mnene basi Bodo akajibanza kwenye kichaka
cha karibu ili ashuhudie vizuri. Wazee wakaanza kuvua nguo huku ngoma zikipigwa
kwa kasi sana. Mara ya kwanza Bodo alidhani wanavua mashati tu. Akatahamaki
kuona walianza kuvua na suruari zao. Bodo akatulia kwenye kichaka chake ili
ashuhudie vyema. Mara wazee wakavua nguo zote wakawa wakicheza kuzunguka mti wa
tambiko. Bodo baada ya kuona hakuna hatari yoyote na wazee walikuwa wakizunguka
tu mti wa tambiko, ujinga wake ukamjia. Akasema aondoke aende kuchekea mbali
kwani ameshashuhudia kila kitu.
Bodo akainuka akaanza kunyata ili aondoke mazingira
yale na kwenda kuangua kicheko chake mbele ya safari. Alipiga hatua ya kwanza
tu, radi ilisikika kwa kishindo kikubwa katika kichaka alichokuwa amejificha.
Ntemi aligeuka kuona kuna nini akaona vipande vya nguo vikiruka kila kimoja
upande wake. Na wakati ule ule radi pia ilipiga nyumbani kwa kina Bodo na
kuwauwa baba yake na mama yake pale pale. Tabia mbaya ya Bodo ikagharimu maisha
ya wazazi wake.
HADITHI
YA 9: MKUTANO WA AKINA MAMA.
Mwanamke ni nguzo ya familia yoyote ile, iwe familia
ya wastaarabu au hata familia ya mabaradhuri. Mwanamke ndiye kiumbe pekee
mwenye uwezo wa kuitengeneza au hata kuibomoa familia na jamii yake. Mvuto wa
mwanamke haupingiki kwa hoja iwayo yote ile kwa sababu akiamua kuiangamiza
familia yake ni muda mfupi tu wanafamilia wataacha majina yao na kuitwa malehemu.
Ratiba ya mwanamke ndiyo ratiba ya familia nzima. Maana kila apangapo ratiba
hufikilia hisia na matakwa ya kila mwanafamilia.
Wanaume wengi wa Kanyaga walikuwa hawajui watakula mlo
gani kila kukipambazuka. Lakini kwa wanawake ilikuwa jambo dogo na hata
walikuwa hawaliwazii kabisa. Walipokuwa wakitenga chakula kila mtu alijikuta
akipata mboga ya mahitaji yake. Kuna ambao hawakupenda kula mrenda walikuwa
wakitengewa maziwa ya mgando kila mrenda ulipokuwa ukipikwa. Kuna wengine
walikuwa hawapendelei maziwa hivyo mboga zikikosekana basi kulikuwa na nyama ya
kukaushwa iliyohifadhiwa kwa muda mrefu darini, maarufu kwa jina la Ng’omele.
Kila mwanafamilia alikuwa akiridhika kila chakula kilipotengwa.
Ratiba za kuanza msimu wa kilimo pia zilikuwa zikipangwa
na wanawake wa familia. Haijawahi kujulikana walipata wapi utashi huo lakini
kila walipofanya maaamuzi ya zao la kulimwa kwa wingi walikuwa sahihi. Wanaume
wengi walikuwa wakijivunia tu magunia yaliyorundikwa gharani bila hata
kuwapongeza wake zao kwa juhudi waliyokuwa wakionesha.
Baadhi ya wanaume walevi walikuwa wakipanga masharti
magumu kwa wake zao. Kwa mfano walikuwa wakitaka kila waliporudi toka ulevini
wawakute wake zao hawajalala hata kama ni usiku wa manane. Wengine walidai
chakula cha moto na kuwalazimisha wake zao kuamka usiku na kuanza shuruba za
kupika chakula kwa ajili yao. Wengine walienda mbali Zaidi kwa kuwageuza wake
zao kuwa ngoma na kuhakikisha wakizipiga kila waliporudi toka ulevini.
Lugandya, mlevi maarufu pale Kanyaga alikuwa ni kinara wa
kumyanyasa mke wake, Nkwaya kwa vipigo. Alikuwa akilewa hurudi na kumlaumu kwa
nini hakumpatia mtoto. Walevi huwa hawana akili kabisa kwa sababu anaweza
kukuuliza swali ukajitahidi kumjibu vizuri yeye akakwambia umemdharau. Basi
mkewe Lugandya akawa ngoma ya kijiji haswa. Kila jioni ni vipigo na mayowe.
Siku moja Lugandya akamwambia mke kuwa anataka kumuolea mke mwenza kwa sababu
yeye tumbo lake lilikosa shukrani.
Nkwaya binti Machota alikuwa ni mke mnyenyekevu kwa
mumewe, akapiga magoti na kumuomba wajitahidi kufuata masharti ya mganga kwa
mwaka mmoja asipompatia mtoto basi aoe mke mwingine. Weee! Sijui maneno gani
yaliingia masikioni kwa mlevi Lugandya. Alimuangushia kipigo cha kiutu uzima.
Akachukua mwichi wa kutwangia akaanza kujpiga nao. Nkwaya ilibidi apige yowe za
kuomba msaada. Majirani walifika kutoa msaada na kumkuta Nkwaya akiwa na hali
mbaya.
Walimchukua Nkwaya na kwenda kumpeleka kwa mganga wa
jadi usiku uleule. Mganga alipomchunguza mgonjwa wake akagundua alikuwa
amevunjia mguu na mkono na alikuwa akitokwa na damu puani na mdomoni. Mganga
alitumia miti shamba yake kwa usahihi na kuzuia damu iliendelee kutoka Zaidi.
Asubuhi iliyofuata mke wa mganga, Mhoja akaanza shughuli ya kutibu mkono na
mguu wa Nkwaya vilivyovunjika. Utaalamu wa kuunganisha mifupa iliyovunjika
Mhoja alichanjiwa na baba yake Nyenye.
Hivyo mganga japokuwa alikuwa akijua miti shamba ya
aina zote lakini alikuwa hajapata bahati ya kuchanjiwa dawa ya kuunga mifupa.
Mganga alikuwa ni mtu mwenye jaziba sana hivyo alikataliwa kuchanjwa dawa ya
kuunga mfupa iliyovunjika kwa sababu mtu aliyechanjiwa dawa ya kuunga mifupa
alikuwa akimpiga mtu kibao au hata ngumi basi mtu yule aliyepigwa huanza kuoza
sehemu aliyopigwa. Hivyo waliokuwa wakichanjwa dawa ile ni watu wapole na wasio
na hasira za karibu.
Nkwaya alipofikisha siku saba akaanza kufanya mazoezi
ya kutembea na kuuonyoosha mkono wake baada ya kupona tu, wazee waliitisha
mkutano wa kijiji na kumuuliza Lugandya sababu ya kutaka kumuua mkewe. Lugandya
alikuwa hana cha maana cha kueleza umma wa Kanyaga kwa hiyo alichapwa viboko
arobaini mgongoni pamoa na kulipa masumule ya ng’ombe mzima ili watu
wale kabla ya kumkabidhi tena mke wake. Lugandya alitii na kutekeleza
aliyoambiwa.
Lakini wengi wa wanawake hawakuridhishwa na adhabu
aliyopatiwa Lugandya kwa sababu alikuwa amekusudia kuua. Kwa maono yao waliona
apokonywe mke ili watu wengine wajifunze kuheshimu wake zao. Lakini hakuwepo wa
kuyaeleza mawazo hayo mbele ya umma wa wanaume wanyanyasaji. Moja kati ya
wanawake ambao hawakuridhishwa na kitendo cha kinyama alichokifanya Lugandya
alikuwa ni Malkia. Hivyo baada ya kuyatambua mawazo ya wanawake wenzake na hali
kandamizi waliyokuwa nayo wanaume wengi pale Kanyaga, akatangaza mkutano wa
wanawake ambao ungefanyika kesho yake Ikulu.
Wanawake wengi walipiga makofi na vigeregere kuona
Malkia ameamua ambacho wengi wao walikuwa wakitamani kwa muda mrefu. Baadhi ya
wanaume walihoji maada ya mkutano ila walijibiwa ni mambo ya wanawake na ndio
maana ya mkutano wa wakina mama la sivyo wangeweza kuelezea palepale tu.
Wanaume walifyata mikia yao na kujipa matumaini wake zao walikuwa watiifu na
wasingeweza kuwaza kupindua familia zao.
Siku ya mkutano kwa Ntemi pakawa hapatoshi. Maana
wanawake walikuja kwa idadi yao kamili. Hata ambao siku iliyopita walidamkia
mashambani leo walikuwa wakwanza kufika na kukaa nafasi za mbele kabisa.
Wanawake waliamua kubanana na kutosha sehemu ile ile iliyokuwa ndogo. Vicheko,
nderemo na vifijo zilijaa pale kwenye mkutano. Kila mwanamke alikuwa anafuraha
kuona hata wanawake waliokuwa wakisemwa ni wapole leo walikuwa wakiongea kwa
furaha na vituko.
Malkia alisimama na kuowasalimia, ‘‘Wanawake wa
Kanyaga hoyeee!’’ wanawake walijibu kwa bashasha na furaha kubwa, ‘hoyeee.!’’
Malkia aliwashukuru kwa mahudhurio ambayo hata hakuyategemea. Aliwaasa wanawake
kuwa wito wake haukuwa jaribio la kupindua uongozi wa waume zao bali kuleta
umoja na mshikamano miongoni mwa wanawake wa Kanyaga. Aliwakumbusha kuwa
wanaume wote walikuwa na sehemu za kwenda kubadilishana mawazo; kwenye bao na
kilabuni. Ijapo baadhi ya wanawake walikuwa wakienda kilabuni ila walikuwa ni Wasimbe.
Hivyo aliwaomba wanawake pia watafute mradi ambao
wangekuwa wakiufanya kwa pamoja ili kubadirishana mawazo huku ukiwaachia faida.
Mhoja, mke wa mganga aliyeheshimika na wengi wa wanawake pale kijijini,
alipendekeza pawepo na shamba kubwa la mahindi ambalo mazao yake yatasaidia
kipindi cha maafa ya njaa, misiba na kadhalika. Wanawake wote walikubaliana na
hoja na Malkia akatoa eneo kubwa kwa ajili ya mradi huo.
Malkia pia alipendekeza kufinyangwa kwa vyungu vya
wanawake wa kijiji ili viweze kusaidia katika matukio ya sherehe na misiba.
Maana kijiji kilikuwa hakina vyungu na kusababisha kipindi cha matukio ya
kijamii kuazima vitu hivyo toka kwa wenyenavyo. Wakati mwingine vilikuwa
vikivunjika na kusababisha hasara kwa mmiliki. Wataalamu wa kufinyanga
walijitolea kuwafundisha wanawake wote kufinyanga ili kazi iwe rahisi.
Wanawake wenye uzoefu mkubwa na familia waliyamimina
maalifa waliyokuwa nayo kwa wenye ndoa changa na wale wasio na uzoefu. Maswali
mengi yahusuyo namna ya kuishi na waume wa ain azote yalipata ufumbuzi
mkutanoni. Wale waliokuwa na uzoefu mkubwa walijitolea kuzizungukia kaya
zilizokuwa zikiyumba na kuwapa mbinu madhubuti. Kipengele hiki kilikuwa na michango
mingi Zaidi lakini kilipewa ufumbuzi madhubuti.
Wanawake wa Kanyaga ama kwa hakika walipanga mengi
ambayo yalileta umoja na mshikamano miongoni mwao. Jioni ilikuwa ikifika hakuna
mwanamke aliyekuwa akikaa upweke kwani kila mtaa ulikuwa na sehemu ya kukutania
na kupiga soga au kutekeleza mradi furani. Mara kila familia ikaanza kuneemeka.
Vyakula ambavyo vilikuwa adimu wanawake hawa walijitahidi kuwawina ili kila mji
ukaonje chakula kile.
Baada ya mwaka mmoja kupita mafanikio yakaonekana
kwenye ghala la chakula la wakina mama wa Kanyaga. Wanaume wakaanza kuwategemea
na kuwaamini wake zao. Vya pombe wote wakawa wakirudi nyumbani mapema na kuacha
hata kuwanyooshea wake zao vidole. Kanyaga ikainuliwa na wanawake huku wanaume
wakiiba mawazo yao na kuanzisha shamba la kijiji. Ama kwa hakika mwanamke ni
nguzo ya familia na jamii yake inayomzunguka.
By James Kalimanzila
By James Kalimanzila